KATIKA kuunga mkono Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi, Taasisi ya Bega kwa Bega na Mama, inatarajia kufanya matembezi ya vijana 3,500 kwa siku nne kuanzia Dar es Salaam hadi Rufiji, mkoani Pwani, ili kumuenzi marehemu Bibi Titi Mohamed.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu wa taasisi hiyo, Fatma Sahran, alisema wameamua kufanya matembezi hayo kama ishara ya kuipongeza UWT kwa kutambua mchango wa Bibi Titi na kumuenzi kwa vitendo.
“Taasisi ya Bega kwa Bega na Mama tunawapongeza UWT kwa kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa Bibi Titi Mohamed, kwetu sisi Bibi Titi Mohamed atabaki kuwa alama na nguzo muhimu ya mafanikio ya mwanamke hapa nchini,” alisema.
Alisema matembezi hayo yanayoanza leo Dar es Salaam, yatajumuisha vijana 3,000 wa Dar es Salaam na 500 wa mkoa wa Pwani, ambapo dhamira yao kuu ni kufika Rufiji, ardhi ya nyumbani ya marehemu Bibi Titi.
Fatma alisema, Bibi Titi ni miongoni mwa wanasiasa walioshuhudia kuunganishwa kwa vyama vya African Association na Shiraz Association muunganiko uliozaa Afro Shirazy Party visiwani Zanzibar Februari 5, 1957 ambapo kupitia mkutano mkuu, Bibi Titi alizungumza na wajumbe.
“Bibi Titi hakuishia hapo, katika mikutano ya TANU, alijenga hoja ya kuondoa vizuizi kwa wanawake wanaokwenda katika mikutano hiyo na kutenganishwa kiukaaji kwa kuwekwa pazia kati yao na wanaume.
“Mengi ameyafanya Bibi Titi na kama ukiamua kuandika, basi utajaza vitabu kwa vitabu, itoshe tu kusema kuwa kamwe hatutasahau mchango wake katika mapambano ya uhuru na haki za wanawake,” alisema.
Bibi Titi alizaliwa Juni, mwaka 1926, jijini Dar es Salaam na alifariki dunia nchini Afrika Kusini Novemba 5, mwaka 2000 katika Hospitali ya Net Care.
Na WILLIAM SHECHAMBO