HATUA ya serikali kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, yameendelea kustawisha uchumi wa wafanyabiashara na wawekezaji nchini, hii ni baada ya mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji ‘Mo’, kuendelea kushika nafasi ya 15 kwa utajiri Afrika.
Mo Dewji ambaye mwaka jana kwa mujibu wa jarida la Forbes alikuwa nafasi ya 15 akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni 1.5, mwaka huu pia ameendelea kuwa katika nafasi hiyo, pamoja na changamoto za janga la Uviko-19, hatua ambayo inahusishwa na mazingira mazuri ya kiuchumi aliyotengeneza Rais Samia Suluhu Hassan, tangu kuingia madarakani.
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani, Dk. Josephat Werema, amesema kuimarika kwa uchumi wa mfanyabiashara Mo Dewji, kunachochewa na maboresho yaliyofanywa na serikali na hivyo kurahisisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Dk. Werema ameeleza hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara maarufu kwa Blueprint, ambao serikali imedhamiria kuutekeleza ili kuvutia wawekezaji nchini, ambapo Rais Samia alipoingia madarakani aliahidi kuifungua nchi kibiashara.
Kwa mujibu wa Dk. Werema, pamoja na mazingira hayo, Tanzania pia imekuwa miongoni mwa nchi chache zilizoweka masharti rafiki kwa uchumi baada ya mlipuko wa janga la Uviko-19, jambo ambalo limefanya shughuli za uchumi kuendelea.
“Wakati ulimwengu unakabiliwa na janga hilo, imeshuhudiwa katika mataifa mengi zikiweka marufuku, yakiwemo ya watu kutotoka nje na hivyo kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo kusababisha mdororo,” amesema.
Amesisitiza kwamba hiyo ni tofauti kwa Tanzania kwani,falsafa za Rais Samia ni kuendelea kukabiliana na ugonjwa huo huku wananchi wakiendelea na shughuli zao.
PROFESA SEMBOJA
Naye, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, amesema mazingira ya biashara yana uhusiano mkubwa na kuimarisha kwa utajiri wa uwekezaji wa bilionea Mo Dewji.
Ameeleza pamoja na mazingira bora ya biashara mambo mengine yanayowafanya wawekezaji wa Tanzania kuimarika ni mazingira yenye uwezo wa ushindani wa biashara na mataifa mengine.
Pia, ameongeza suala la matumizi mazuri ya mikopo kutoka taasisi za fedha ni moja ya mambo linalowafanya kuimarika.
MO DEWJI
Miongoni mwa biashara alizowekeza Mo Dewji nchini ni za viwanda vya vyakula, vinywaji, usafiri na pia Mo Foundation inatoa misaad mbalimbali ya kijamii, huku pia mfanyabiashara huyo akiwa ni mwekezaji katika klabu kubwa ya Simba.
Mo amekuwa ni mmoja wa matajiri vijana wanaofanya vuziri barani Afrika, na amekuwa akitoa maelfu ya ajira kwa Watanzania.
NA JUMA ISSIHAKA