RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya kwamba, wakati wowote kuanzia sasa atawang’oa mawaziri wote wasiotumikia wananchi na badala yake wanawaza siasa za 2025.
Mkuu wa nchi alitoa onyo hilo jana Ikulu, Dar es Salaam wakati akipokea Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, ambapo alisema serikali imedhamiria kufanya kazi ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Alisema wakati alipokabidhiwa nafasi ya Urais, alitembelewa na mmoja wa wazee, ambaye alimpa pole kwa nafasi hiyo aliyopewa, huku akimueleza kuwa atakabiliana na upinzani mkubwa kutoka kwa watu wanaovaa mashati ya kijani.
‘’Nilipokabidhiwa huu mzigo, nilianza kusikia lugha zinasema serikali ya mpito,serikali ya mpito Bungeni huko kwa kina Kassim, nikarudi kwenye Katiba kuangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi, sikuona, nikasema anhaa, twendeni,” alisema Rais Samia na kuibua shangwe kwa wahudhuriaji wa hafla hiyo, wakiwemo Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mikoa, ambapo aliwaambia hata wao wameanza kupanga safu za Wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Aliongeza:’’Nimenuia kuleta maendeleo lakini yanayojitokeza sasa ni ‘stress’ za 2025.Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini na kumpa dhamana ya kushika mhimili, anakwenda kusimama na kusema yale. Ni ‘stress’ ya 2025.
Walitaka kunijaji kwa kunitazama, ‘Don’t judge a book by its cover, walitaka kunijaribu, hapa kwangu wamekosea.” alisema Rais Samia huku akitangaza rasmi kuwa atafanya mabadiliko ya baraza la mawaziri ili kuwaondoa mawaziri wenye nia za 2025, ili wakafanye yao kwani wameshindwa kutumikia wananchi.
Alisema alipofanya mabadiliko madogo ya mawaziri alitangaza kuwa hapo ni mwanzo na atafanya mabadiliko zaidi, hivyo kuanzia sasa muda wowote atafanya mabadiliko ya mawaziri ili kuwatoa wote wanaowaza siasa za 2025 kwenda kuzifanya kwa kuwa yeye kwa sasa anafanya maendeleo ya wananchi.
‘’Mimi ni mtu wa maendeleo na ndio maana nimeanza sasa kufanya juhudi za kuwakwamua wananchi, ningekuwa ni mtu wa kuwaza siasa za 2025 nisingefanya mambo makubwa sasa bali ningesubiri 2023 kwa kuwa ni karibu na 2025. Yote haya yanayofanyika ni kwa ajili ya wananchi,’’ alisema.
Aliongeza, ‘’Moyo wangu sio wa glasi, nina moyo wa nyama ulioumbwa na Mwenyezi Mungu. Nishikeni mkono tuendelee pamoja kuleta maendeleo. Tutafanya mabadiliko ili tulete maendeleo ya wananchi na wanapaswa kuamini kuwa uongozi unaletwa na Mwenyezi Mungu’’.
Rais Samia alisisitiza, “Nitatoa list (orodha) mpya karibuni ya wale wote, ninahisi wanaweza kwenda na mimi nitakwenda nao, wale ninaohisi ndoto zao ni kule nitawapa nafasi waende wakajitayarishe vizuri huko nje, sababu nikiwatuma ndani nitawasumbua na ndio maana wanafanya ya kwao,’’ alisema.
Hivyo, Rais Samia alitaka utendaji kazi wa bidii ili kuleta maendeleo makubwa kwa nchi na kuwa watanzania wanataka maendeleo na serikali imedhamiria kuyaleta kwa kasi kubwa, kupitia tozo na mikopo wanayochukua nje ya nchi kwa dhumuni kuu la kuharakisha maendeleo.
NA HAMIS SHIMYE