MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imetupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa la kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo na wenzake kwa kupitia mawakili wao wamewasilisha pingamizi lingine Mahakamani hapo wakipinga hati ya mashitaka wakidai ina kasoro za kisheria.
Hayo yalijiri jana Mahakamani hapo mbele ya Jaji Elinazer Luvanda, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutolewa uamuzi wa iwapo Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ama la.
Akitoa uamuzi huo uliotokana na pingamizi la awali lililowasilishwa na Mbowe na wenzake kupitia jopo la mawakili wao 14 wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, Jaji Elinazer alisema Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ugaidi, hivyo haikubaliani na pingamizi hilo.
Jaji Elinazer alisema anakubaliana kwamba pale panapokinzana kati ya sheria ya jumla na sheria mahsusi basi sheria mahsusi inapewa kipaumbele.
“Sheria namba tatu ya ugaidi inatoa tafsiri ya Mahakama kuwa ni Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Zanzibar, kifungu namba 21 na 22 cha sheria hiyo havikufanyiwa mabadiliko, pia makosa ya ugaidi yakichotwa na kuwa makosa ya uhujumu uchumi hivyo inalazimu kufuata mkondo mwingine kwa mazingira yaliyomo katika shauri hilo na kuleta suluhisho,” alisema.
Alisema kwa kufanya marejeo kifungu namba 107 cha Sheria ya ardhi kabla ya marekebisho, mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ardhi ilipewa Mahakama Mahsusi ya Ardhi na kuondolewa mamlaka mahakama zingine na kwamba sheria ya kazi pia imetoa mamlaka kwa Mahakama ya Kazi.
Jaji Elinazer alisema kama ingekuwa sheria namba 21 ya mwaka 2002 au sheria namba 3 ya mwaka 2016 ingetoa mamlaka mahsusi kwa mahakama fulani kusikiliza mashauri chini ya sheria ya ugaidi, hoja ya pingamizi ingekuwa na nguvu.
Alisisitiza kuwa sheria hizo zinatoa mamlaka mahsusi ya kusikiliza mashauri ya ugaidi, hivyo hoja haina mashiko.
Agosti 30, mwaka huu, waliwasilisha pingamizi la awali likiwa na sababu nne kupinga usikilizwaji wa shauri hilo likiwemo la kwamba Mahakama hiyo, haina mamlaka ya kusikiliza makosa yaliyofunguliwa chini ya sheria ya ugaidi.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulipinga hoja hizo na kudai Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, upande wa Jamhuri ulitaka kuwasomea washitakiwa mashitaka na maelezo ya awali, hata hivyo Wakili Kibatala, alipinga kwa kuwasilisha pingamizi la awali likiwa na hoja tatu wakidai hati ya mashitaka ni batili. Kibatala alidai shtaka la kwanza halielezi ni kwa namna gani ugaidi umetokea.
Alidai Mahakama haina mamlaka ya kuendesha mashitaka yanayowakabili washitakiwa wote kwa sababu kifungu cha 4 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002, ambacho ndicho kinaweka zuio zaidi la makosa ya ugaidi nchini, hakifafanui ni vitu gani au viashiria gani vinavyotengeneza ugaidi.
Pia, alidai katika mashitaka ya kula njama ya kutenda kosa na la kushiriki mkutano lilipaswa kuwa shtaka moja.
Alidai mashitaka hayo mawili yanapaswa kuondolewa katika hati hiyo kwa sababu yanakwenda kinyume na utaratibu na yana kasoro zisizorekebishika, hivyo aliiomba Mahakama hiyo kutokubaliana na mashitaka hayo na kuyaondoa.
Baada ya kuwasilisha mapingamizi hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, aliiomba mahakama iwape muda wa kuyapitia ili kuwasilisha majibu yao.
Jaji Elinazer alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha shauri hilo hadi kesho ambapo upande wa Jamhuri utawasilisha majibu ya mapingamizi hayo na kutolewa uamuzi.
Mbali na Mbowe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adamu Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Ling’wenya.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita yakiwemo ya kula njama kutenda makosa ya ugaidi.
Na SYLVIA SEBASTIAN