MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imetupilia mbali mapingamizi yaliyowasilishwa na mawakili wa utetezi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na kuamua kupokea maelezo ya onyo ya mshitakiwa Adam Kasekwa kama kielelezo cha upande wa Jamhuri.
Aidha, Jaji Kiongozi Mustapher Siyani, ametangaza kujitoa kusikiliza shauri hilo kwasababu ya majukumu mpya aliyonayo huku akieleza kuwa uhasilia wa kesi hiyo inatakiwa kusikilizwa mfululizo, ili kujulikana hatima yake.
Hayo yalijiri mahakamani hapo, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutolewa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi wa ama kupokelewa au la maelezo ya onyo yanayodaiwa kutolewa na mshitakiwa Kasekwa.
Kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ilitokana na upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala, kupinga kupokelewa kwa maelezo hayo kwa madai kabla na baada ya kuchukuliwa mshitakiwa aliteswa na yalichukuliwa nje ya muda kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Mbowe na Kasekwa, washitakiwa wengine katika kesi ya msingi ni Mohamed Ling’wenya na Moses Lijenje, wanaokabiliwa na mashitaka ya
Ugaidi.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Kiongozi Siyani alisema anapokea maelezo hayo kwasababu ushahidi wa upande wa utetezi uliotolewa mahakamani hapo hauendani na pingamizi lililowasilishwa.
Kuhusu hoja ya kwamba maelezo yalichukuliwa nje ya muda, Jaji Kiongozi Siyani alisema maelezo yalichukuliwa ndani ya muda ambao askari waliutumia kumtafuta mtukumiwa Lijenje aliyekuwa na Kasekwa.
Pia, alisema hakuna ubishi kwamba washitakiwa hawakukataa walikuwa na Lijenje katika eneo la tukio, Rau Madukani Moshi, ambapo askari walifanikiwa kuwakamata washitakiwa (Kasekwa na Mohamed Ling’wenya), badala ya watatu jambo lililowalazimu kushirikiana na polisi kumtafuta Lijenje.
Alisema katika kesi hiyo, polisi walikuwa na sababu ya kuchelewa kuchukuwa maelezo ya mshitakiwa kwa kuwa shughuli za kiupelelezi zilizokuwa zikiendelea na kumtafuta Lijenje na kuwasafirisha watuhumiwa kutoka Moshi hadi Dar es Salaam.
Katika hoja ya kwamba maelezo yalichukuliwa mshitakiwa akiwa katika mateso, Jaji Siyani alisema mshitakiwa alikubali kutoa maelezo, lakini hakuna ushahidi wa kwamba hakufika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam, yalipochukuliwa maelezo hayo.
Alisema katika ushahidi wa upande wa utetezi, hakuna mahali upande huo ulibainisha Kasekwa hakufika kituo hicho cha polisi.
Jaji huyo alieleza kuwa wakati shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Ramadhan Kingai akitoa ushahidi wake aliieleza Mahakama kwamba maelezo ya onyo ya Kasekwa yalichukuliwa kituoni hapo kuanzia saa moja na nusu hadi saa tatu asubuhi, lakini hakuna panapobishaniwa kuwa hakufika kituoni hapo.
Alisema maelezo ya shahidi yanakinzana na hoja ya msingi ya kuteswa kwake na kwamba hakuna ubishi kuwa Kasekwa alitoa maelezo kwa ridhaa yake na kwa hali hiyo, hivyo ameyapokea maelezo hayo kama kielelezo namba moja cha upande wa Jamhuri.
Kasekwa katika ushahidi wake mahakamani hapo, alikana kuongoza askari kumtafuta Lijenje, kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kati Agosti 7, mwaka 2020 na alipelekwa kituo cha Polisi Tazara kisha Mbweni na waliomkamata walimtesa na alilazimishwa kutoa maelezo na kutia saini nyaraka akiwa Mbweni Agosti 9, mwaka 2020.
JAJI AJITOA
Akitangaza uamuzi wa kujitoa kusikiliza kesi hiyo, Jaji Siyani alisema amefikia uamuzi huo kwasababu ya majukumu mpya aliyonayo huku akieleza kuwa kwa uhasilia wa kesi hiyo inatakiwa kusikilizwa mfululizo, ili kujulikana hatima yake.
“Kutokana na majukumu haya sitaweza kusikiliza, hivyo naona ni busara kujitoa ili msajili wa Mahakama ampangie Jaji mwingine ambaye ataendelea pale alipoishia.”
“Nawashukuru wote mliokuwa mkihudhuria kesi hii kwa kipindi chote kwa kusikiliza. Hivyo najitoa rasmi na msajili atapanga jaji atakayesikiliza, jina la Jaji atakayekuja na tarehe msajili atasema,” alisema.
Jaji Kiongozi Siyani alisema kesi hiyo itakapopelekwa tena mahakamani hapo inatarajiwa kuendelea kwa ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri Kingai aendelee kutoa ushahidi wake pale alipoishia.
Hivi karibuni Jaji Siyani aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jaji Kiongozi akichukuwa nafasi ya aliyekuwa Jaji Kiongozi, Eliezar Fereshi, aliyeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Huyo ni Jaji wa pili kujitoa kusikiliza kesi hiyo, ambapo Jaji wa kwanza alikuwa Elinaza Luvanda ambaye alijitoa baada ya washitakiwa kumuomba afanye hivyo kwa kuwa hawakuwa na imani naye.
Askofu afanya maombi mahakamani
Kabla Jaji Siyani hajaingia mahakamani na kesi kuanza kusikilizwa, Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Uamsho, Emmaus Mwamakula alifanya maombi kwa kuwaombea washitakiwa hao pamoja na mawakili wa utetezi.
Askofu huyo alifanya maombi kwa kuanza kuombea jopo la Mawakili wa utetezi na baadaye Mbowe na washitakiwa wenzake walipoingizwa ndani ya chumba cha mahakama pia aliwaombea.
Maombi hayo yalifanyika kwa mawakili hao kusimama kwa pamoja na askofu huyo huku wakionekana kuinamisha vichwa kwa dakika kadhaa.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama kutenda makosa ya ugaidi, kukutwa na mali iliyokusuduwa kutumika kutenda vitendo vya kigaidi na kufadhili vitendo vya kigaidi linalomkabili Mbowe.
NA REHEMA MOHAMED