MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM) amembatiza jina Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa Afisa Ugani Mkuu nchini kutokana na uhamasishaji anaoufanya kwenye sekta ya kilimo.
Hilo limejitokeza bungeni wakati, Mbunge huyo akichangia mjadala wa mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2022/23.
Mtaturu amesema kwenye eneo la uwekezaji wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji mpango haujaeleza Serikali imejiandaaje kuwasaidia wakulima.
“leo ukienda kila halmashauri inaongelea upungufu wa maafisa ugani ambao ni wataalam leo wakulima wengi wanalima kilimo cha kurithi, kilimo cha mazoea ambacho mtu anapata debe mbili tatu kwenye heka moja kitu ambacho anapoteza muda.
“Eneo hili mpango uweze kubainisha bayana namna gani tunaweza kutoka kumsaidia mkulima kule kijijini aweze kutoka kupitia kilimo, nimpongeze Waziri Mkuu namna amejitahidi kupita mahali kuhamasisha kilimo, anahamasisha kilimo katika maeneo mbalimbali Spika katika eneo la kilimo amesaidia sana,”alisema Mtaturu.
Aliongeza: “Na mimi ndio maana nimembatiza kuwa yeye ndio afisa ugani Mkuu katika nchi yetu, anafanya kazi nzuri ya kuhamasisha kilimo pasipowezekana panawezekana namna ambavyo anakaa na sisi, ushahidi ninao amekuja Singida amekaa na sisi siku nzima bila ya kutoka kwenye kiti tukaweka mkakati ambapo zao la alizeti litaenda kusaidia nchi katika mafuta ya kula nampongeza na sisi kama wabunge tunaiomba serikali iongeze fedha kwa ajili ya kuhakikisha maeneo hayo tunaenda vizur.”
Na SELINA MATHEW, DODOMA