MCHANGO wa sekta ya madini katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 7.7 mwaka huu, lengo likiwa kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, wakati akiwasilisha mada katika mkutano wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) katika kujadili mchango wa Azaki katika maendeleo ya nchi.
Alibainisha kuwa mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa umeimarika kufikia asilimia 7.7 mwaka huu suala ambalo limechangiwa na usimamizi thabiti wa shughuli za madini nchini.
“Mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa ulikuwa asilimia 3.4 mwaka 2015, asilimia 5.2 mwaka 2019, asilimia 6.7 mwaka 2020 na sasa umeongezeka mpaka kufikia asilimia 7.7, tunaamini ifikapo 2025 mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa utakuwa umekafikia asilimia 10,” alisema.
Biteko alieleza kuwa mabadiliko ya Sheria ya Madini sura namba 123 ya Mwaka 2017 yamesaidia kwa kiwango kikubwa kuwafanya Watanzania kushiriki katika uchumi wa madini, ambapo katika kipindi cha mwaka 2020/2021 jumla ya kampuni za watoa huduma migodini 961 sawa na asilimia 66 zilikuwa ni za Kitanzania.
Alieleza kuwa uwepo wa idadi kubwa ya watoa huduma wa Kitanzania umechochewa kwa kiasi kikubwa na usimamizi wa Sheria ya Madini na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.
Alibainisha kuwa wizara imekuwa ikisisitiza wamiliki wa leseni za madini kutoa kipaumbele kwa bidhaa au huduma zinazotolewa na Watanzania kwa kuhakikisha kuwa bidhaa au huduma pekee zinazotolewa na kampuni za kigeni ni zile ambazo hazipatikani nchini.
Biteko alisema baada ya Uhuru, Watanzania walikuwa na kiu ya kuona rasilimali madini zinawanufaisha, ndiyo maana aliyekuwa Rais wa kwanza Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema madini tusichimbe mpaka tutakapopata wataalam wazawa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Stephan Byabato, alisema wizara hiyo mpaka sasa imeshatembelea maeneo yote ambayo bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani mkoani Tanga litapita, kubaini mahitaji watakayoweza kuyapata katika maeneo husika kwa ajili ya kutimiza Sheria ya Ushirikishwaji wa Wazawa.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma