WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, amesema hatawasaliti watumishi wa umma wanaofanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo kwa taifa.
Kauli hiyo aliitoa mkoani Kigoma, alipokuwa akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa mkoa huo.
Aliahidi kwamba atahakikisha anasimamia haki na stahiki za watumishi wa umma nchini, kwa lengo la kuwaongezea morali ya utendaji kazi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.
Kutokana na hilo, Mchengerwa alitoa rai kwa watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, ili kuendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan, badala ya kufanya kwa mazoea kwa kuwa wasipowajibika hatakuwa tayari kutetea stahiki zao.
“Pale ambapo tutabaini kuna mtumishi mzembe, mla rushwa na mbadhirifu wa mali za umma sitakuwa tayari kumtetea, lakini nitakuwa tayari kupambana na kumtetea mtumishi yeyote muadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa taifa lake muda wote asubuhi, mchana, jioni na usiku,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa aliwaelekeza watendaji kufuatilia utendaji kazi wa watumishi walio chini yake kuongeza ubunifu katika eneo lake la kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndiyo walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma nchini.
Aidha, aliwataka waajiri kutenga bajeti ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa umma walio katika maeneo yao, ili waweze kuwa na weledi, ubunifu na kuongeza ufanisi kiutendaji.
Waziri Mchengerwa yuko katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo, yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
NA MWANDISHI WETU, KIGOMA