MKUU wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge, amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo, wawe wamekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Agizo hilo alilitoa wakati wa mkutano na wakuu wa shule za sekondari, watendaji wanaosimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa na baadhi ya wafanyabiashara wenye zabuni za ujenzi na vifaa katika Manispaa ya Bukoba.
Alisisitiza hadi ifikapo Novemba 30, mwaka huu, vyumba vyote vya madarasa viwe vimekamilika na kuonya asitokee mtu wa kukwamisha au kuwepo sababu za aina yoyote zitakazosababisha ujenzi kutokamilika kwa wakati.
“Tunapopewa kazi ya muda mfupi tuitekeleze kwa wakati. Kila mmoja wetu asikae ofisini, nimeshatoa maagizo kwa wakuu wa wilaya, kila siku saa 12:00 jioni watoe taarifa ya ujenzi kwangu kuhusu vibarua walioko eneo la ujenzi, idadi ya mafundi na vifaa vilivyotumika,” alisema.
Meja Jenerali Mbuge, aliwahakikishia wakuu wa shule kuwa, watapata fedha kwa wakati, badala ya kwenda halmashauri kupoteza muda na kuwahimiza walimu kusimamia ujenzi kwa uaminifu, kwa wale watakaopata changamoto, ofisi yake iko wazi wafike kwa utatuzi ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati.
Aidha, aliwatahadharisha wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa kiholela, kuacha tabia hiyo huku akitolea mfano Halmashauri ya Misenyi, ambako bei ya saruji imepanda kutoka sh. 21,000 hadi sh. 23,000.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba, Fatina Laay, alisema halmashauri yake ilipokea sh. bilioni 1.7 za ujenzi wa vyumba vya madarasa 85, lakini kilichowakwamisha ni nondo ambazo ziko njiani kupelekwa na vifaa vingine, yakiwemo mabati, saruji na vigae ambavyo vimeagizwa moja kwa moja kutoka kiwandani.
Mkoa wa Kagera ulipokea fedha za Uviko-19 zaidi ya sh. bilioni 20 za ujenzi wa miundombinu ikiwemo vyumba vya madarasa 881.
NA ALODIA BABARA, Bukoba.