WATU watatu wakiwemo viongozi wawili wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Karagwe na Kyerwa, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera, kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kukisababishia chama hicho hasara ya sh. bilioni 7.6.
Washitakiwa hao ni meneja wa chama hicho, Oscar Dominick, mhasibu mkuu Juvenary Burchad na mfanyabiashara Allan Mugisha.
Oscar na wenzake walifikishwa mahakamani hapo kwa kesi tofauti na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Janeth Masesa.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka na Mawakili wa Serikali Juma Mahona na Juma Masanja huku wakitetewa na Mawakili wa utetezi, Aaron Kabunga na Peter Matete.
Akiwasomea mashitaka Wakili wa Serikali, Juma Masanja, alidai washitakiwa Dominick na Burchad, wanadaiwa kati ya Aprili mosi, 2018 na Oktoba 26, mwaka huu, walikula njama na kukisababishia chama hicho hasara ya sh. bilioni 7.6.
Mfanyabiashara Mugisha anadaiwa kufanya biashara ya kahawa bila leseni, kughushi, kuzuia shughuli za kodi, kushindwa kupata na kutumia mashine ya EFD, kushindwa kuomba usajili wa mlipa kodi anayelipa ongezeko la thamani VAT na utakatishaji fedha.
Mugisha anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari Mosi, 2015 na Oktoba 26, mwaka huu, katika maeneo tofauti mkoani Kagera na alifanyabiashara kupitia kampuni ya Kagera Commodity Trading, hivyo kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kukwepa kulipa kodi sh. bilioni 3.4.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Washitakiwa hao walipelekwa mahabusu hadi Novemba 19, mwaka huu, kesi itakapopelekwa kwa kutajwa.
Na Alodia Babara, Bukoba