MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu mfanyabiashara Ramadhani Kimbanga, kutumikia kifungo cha miezi sita jela, baada ya kumtia hatiani kwa makosa mawili, likiwemo la kusababishia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), hasara ya zaidi ya sh. milioni 16.2.
Mshitakiwa huyo alipewa adhabu hiyo Mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega.
Akisoma adhabu hiyo, Hakimu Janeth alisema Mahakama hiyo inamtia hatiani mshitakiwa kama alivyoshitakiwa, baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri ambao ni askari watatu na ofisa kutoka TTCL.
Amesema kwa mujibu wa shahidi wa kwanza na wa pili, walimkuta mshitakiwa akiiba nyaya za TTCL zinazotumika kutoa huduma muhimu hapo kwa hapo, hivyo walimkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Buguruni.
Hakimu huyo aliendelea kuchambua ushahidi kwa kusema mshitakiwa huyo alifikishwa kituoni hapo akiwa na nyaya na kebo, ambapo kwa mujibu wa ofisa kutoka TTCL, uharibifu huo uliisababishia mamlaka hiyo hasara ya sh.16,222,298.
Aliongeza kuwa upande wa Jamhuri pia wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, uliwasilisha Mahakamani hapo vielelezo miwili ambavyo ni nyaya zilizoibwa na mshitakiwa na risiti ya gharama za matengenezo kutokana na wizi uliofanywa.
“Kutokana na ushahidi uliowasilishwa Mahakamani na upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa pasi na kuacha shaka yoyote, hivyo namtia hatiani katika mashitaka yote mawili,” alisema
Mashitaka hayo ni kuharibu miundombinu inayotumika kutoa huduma muhimu na la kuisababishia mamlaka husika hasara ya sh. 16,222,298.
Hakimu Janeth alisema Mahakama kwa uzingatia shufaa ya mshitakiwa inampa adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kila kosa, ambapo adhabu hiyo itakwenda pamoja.
Alisema Mahakama inatoa adhabu hiyo ikizingatiwa kwamba mshitakiwa ameshakaa mahabusu kwa miaka mitatu na anategemewa na ni mkosaji wa mara ya kwanza.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Mosie Kaima, aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa kwa kuwa kitendo alichokifanya siyo tu kinaisababishia hasara TTCL, bali taifa kiuchumi kwa kuwa mawasiliano ndiyo kila kitu.
Na REHEMA MOHAMED