WAKALA wa Barabara nchini TANROADS Mkoa wa Simiyu na Shinyanga wametakiwa kuendelea kuifanyia uchunguzi barabara inayounganisha mikoa hiyo miwili kupitia Maswa Mwigumbi yenye urefu wa km 50.5 ambayo awali ilijengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika kwa asilimia 100 na kubainika kuwa na mapungufu mengine ambayo yatamlazimu mkandarasi kuifumua na kuifanyia marekebisho.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akiikagua barabara hiyo ambayo ujenzi wake katika baadhi ya maeneo unarudiwa kutokana na kugundulika kuwa imejengwa chini ya kiwango.
Aidha, Mhandisi Kasekenya amekisisitiza uchunguzi zaidi ufanyike ili endapo kutakuwa na mapungufu makubwa katika barabara hiyo, irudiwe ikiwemo ukaguzi wa madaraja yaliyopo katika barabara hiyo.
“TANROADS, mikoa ya Simiyu na Shinyanga muendelee kubaini mapungufu mengine kabla huyu bwana hajaondoka, kama tumeona aliweza kuweka ‘material’ ambazo si sahihi basi yawezekana hata madaraja yakawa siyo mazuri, yawezekana kuna mahali pengine ambapo wenzetu wa maabara hawakuona wao kwa muda wao…
Mkisaidiana na hawa wahandisi washauri, muendelee kuyabaini … kuna maeneo mengine ambayo yamegundulika mapya kabisa ambayo mwanzoni hayakuonekana, kwahiyo inawezekana asilimia kubwa barabara hii ikafumuliwa”. Amesema Mhandisi Kasekenya.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kasekenya ametoa maelekezo ya kufanyiwa uchunguzi wa kutosha kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hususan ya barabara kabla ya kuanza kazi , huku akitaka wakandarasi wote wanaofanya ujenzi wa miradi mbalimbali ya barabara nchini kutumia vizuri wataalam wao na wasisubiri kusimamiwa.
“Mkandarasi huyu achunguzwe vizuri kila anapopewa kazi kwa sababu anaweza kuwa na sifa, wachache wale wamemuharibia lakini kwa kuwa hili limeonekana kila anapopewa kazi afanyiwe uchunguzi wa kutosha.
wakandarasi wote wawe wa nje na wa ndani , wao wana wataalam, kuna michoro, kuna maelekezo na kuna viwango ambavyo vingefuatwa hapa tusingefika, lakini kuna suala la kutumia ‘materials’ maana yake kama unatakiwa kuweka kokoto ukaweka mfinyanzi ‘definetly’ hiyo barabara itakuwa ni mbovu yote na hapa ndicho tunachokiona” ameongeza mhandisi Kasekenya.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya KYONG DONG ya nchini Korea Kusini, Mazige Self, ameeleza ujanja ujanja uliokuwa ukifanywa katika ujenzi wa barabara hiyo ambapo amesema udongo uliokuwa ikitumika sio rafiki sambamba na ushindiliaji .
“Walikuwa wakija watu wa TANROADS wanawaonesha eneo wanalotoa udongo maalum kwa ajili ya shughuli hiyo lakini wakiondoka (TANROADS) wanakwenda kuchukua udongo sehemu nyingine ambao sio rafiki kwa ujenzi lakini pia ushindiliaji ulikuwa sio mzuri” amesema Mhandisi Mshauri Self .
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi John Mkumbo, amesema jumla ya km 5.1 zilitakiwa kurudiwa ambapo tayari km 3.7 zimeshakarabatiwa huku akiongeza wataendelea kusimamia hatua kwa hatua lengo likiwa kufuata taratibu sahihi za ujenzi.
Na Anita Balingilaki, Simiyu