SERIKALI imesema katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, inajivunia kuona idadi ya Watanzania wanaomiliki ardhi imeongezeka kutoka 26,499 kabla ya Uhuru hadi kufikia 2,067,044.
Imesema kwa kutambua umuhimu wa kuboresha makazi ya wananchi ilianzisha kampuni ya kutoa mikopo ya gharama nafuu kwa benki ili wananchi wakope fedha za ujenzi wa nyumba.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliyasema hayo jijini Dodoma, alipokuwa akitoa mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru ya wizara hiyo.
Lukuvi alisema tangu Uhuru hadi sasa serikali inajivunia kuona wananchi wake wanaishi katika makazi bora zaidi ikilinganishwa na kabla ya Uhuru.
“Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru tuna miliki za ardhi 2,067,044, vyeti vya ardhi ya kijiji 11,744 na hati za hakimiliki za kimila 867,148 zimetolewa,” alisema.
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa: “Leseni za makazi 112,787 zimetolewa kwa wananchi waishio maeneo yasiyopangwa mijini na baadhi ya wananchi wanazitumia hati hizo kama dhamana kupata mikopo katika taasisi za fedha kwa shughuli za kiuchumi.”
KUBORESHA MAKAZI
Lukuvi alisema baada ya kupata Uhuru mwaka 1961, serikali ilianza kuboresha mazingira ya uendelezaji milki nchini na kuanzisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Aliongeza kuwa mwaka 1992, serikali ilianzisha Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali ili kuwasaidia kupata mikopo yenye masharti nafuu ya kujenga nyumba za kuishi.
Waziri alisema hadi sasa serikali imetoa mikopo ya nyumba yenye thamani ya sh. 9,159,902,229.85 kwa watumishi takriban 1,689.
“Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuboresha makazi ya wananchi ilianzisha kampuni ya kutoa mikopo ya gharama nafuu kwa benki ili kuwezesha wananchi kukopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Hadi sasa taasisi za kifedha 32 zinatoa mikopo kwa wananchi,” alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema serikali imeshatoa sh. bilioni 474.5 za kuwawezesha wananchi katika ujenzi wa nyumba, lengo ni kuboresha ustawi wa jamii katika maeneo ya vijijini.
UPIMAJI ARDHI
Kuhusu upimaji ardhi, Waziri Lukuvi alisema mafanikio makubwa zaidi yaliyopatikana katika masuala ya upimaji ni upatikanaji wa vifaa vya kisasa na usimikaji wa miundombinu ya kisasa ya upimaji yenye kurahisisha upimaji.
Alisema kwa sasa kuna kasi kubwa ya upimaji wa ardhi na utoaji wa hati miliki kwa kuwa wamezingatia vifaa vya kisasa vya kuandalia ramani za msingi kwa ajili ya kuwezesha utayarishaji na uchapaji ramani.
Alibainisha kuwa serikali imenunua ndege isiyokuwa na rubani maalumu ya upigaji picha za anga zinazowezesha uandaaji wa ramani za msingi na kuzifanyia marejeo.
“Kutokana na mfumo na vifaa vya kisasa, viwanja 2,783,278 na mashamba 28,784 yamepimwa nchini kote na kwa sasa kasi imeongezeka zaidi, tumepeleka sh. bilioni 50 katika halmashauri nchini kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi,” alisema Lukuvi.
SAKATA LA MADALALI
Waziri Lukuvi alisema Desemba 13, mwaka huu, anatarajia kukutana na madalali wa nyumba na viwanjaa jijini Dar es Salaam ili kupanga mikakati ya namna watakavyotekeleza majukumu yao.
Alisema hali hiyo inatokana na mwenendo wa ufanyaji kazi umekuwa si wa kuridhisha na kuzua taharuki kwa jamii.
“Nitakutana nao ili tuangalie mustakabali wa suala lao, naamini hapa hakuna kinachoshindikana kila kitu kitakuwa sawa tunataka kila mtu afanye kazi yake kwa usahihi,” alisema Lukuvi.
UTATUZI WA MIGOGORO
Lukuvi alisema baada ya Uhuru, utatuzi wa migogoro ya ardhi ulikuwa unafanyika kupitia mabaraza ya kimila na mfumo wa mahakama za kawaida.
Hata hivyo, utatuzi wa migogoro ya ardhi kupitia mfumo wa mahakama ulibainika kuwa na changamoto za mlundikano wa mashauri na matumizi ya mbinu nyingi za kisheria.
“Kutokana na kukithiri kwa migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya makundi mbalimbali nchini serikali iliunda kamati ya mawaziri ya kisekta ya wizara nane mwaka 2018, inayojumuisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Maliasili na Utalii; Mifugo na Uvuvi; Kilimo; Maji; na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo na kuridhiwa na Baraza la Mawaziri, Septemba, 2019 ni kuhalalishwa rasmi kwa vijiji 920 kati ya vijiji 975 vilivyokuwemo ndani ya hifadhi, mapori ya akiba na ranchi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na kijamii.”
Waziri lukuvi alisema ili kupunguza migogoro ya ardhi wameanzisha mfumo wa kielektroniki, ambapo mtu akiomba kiwanja itaonyesha katika mfumo kama kinamilikiwa na mtu au la.
Hatua hiyo imekuja baada ya kubaini chanzo cha migogoro mingi na kutolea mfano Dodoma, inasababishwa na utoaji umiliki sehemu moja kwa watu tofauti zaidi ya mmoja.
PATO LA TAIFA
Kwa mujibu wa waziri huyo, umilikishaji wa ardhi kwa wananchi umewapa fursa wananchi kuchangia pato la Taifa.
Alisema serikali inakusanya maduhuli ya sekta ya ardhi kutoka katika vyanzo mbalimbali kama vile kodi ya Pango la Ardhi, Ada za Upimaji wa Ardhi na Machapisho mbalimbali Ada ya Uthamini, Ada za Usajili wa Hati na Nyaraka Mbalimbali.
Waziri alisema kwa miaka 10 ya hivi karibuni Juni, 2011 hadi Jalai, 2021 wamekusanya sh. bilioni 735.8, hivyo maduhuli yatokanayo na sekta ya ardhi yameongezeka kutoka sh.bilioni 1.4 kwa mwaka wa fedha 1996/97 hadi kufikia sh. bilioni 121 katika mwaka wa fedha 2020/21.
“Na kwa mwaka huu (2021/2022) tuna malengo ya kukusanya bilioni 221. Matarajio ni kuhakikisha sekta hii inachangia zaidi katika pato la Taifa ikiwemo mapato ya kodi,” alisema.
NA FRED ALFRED DODOMA