WIZARA ya Madini imeendelea kufanyia kazi maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu kudhibiti utoroshaji na wizi wa madini migodini kwa kuweka miundombinu ya kudhibiti wizi huo.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukuru Manya, katika sherehe za ufungaji wa maonyesho ya nne ya teknolojia na uwekezaji katika uwekezaji sekta ya madini, yaliyofanyika mkoani Geita.
Profesa Manya alisema Rais Samia alitoa maelekezo juu ya kuangalia upya ufanyaji wa biashara ya madini ya Tanzanite katika mgodi wa Mirerani, mkoani Manyara, kazi ambayo inatekelezwa na wizara hiyo.
Profesa Manya alisema kutokana na maelekezo hayo, wametoa maelekezo ya shughuli za madini hayo kufanyika katika eneo hilo badala ya kupelekwa maeneo mengine ili mgodi huo uwanufaishe wananchi wa eneo hilo.
“Tunaendelea kuimarisha mifumo ya kuzuia utoroshaji wa madini…kwa mfano tumeanzisha masoko ya madini na viwanda vikubwa vya kuongeza thamani madini vinakuja, ili kuhakikisha madini yote yanayochimbwa yanaongezezwa thamani nchini,” alisema.
Profesa Manya alisema kuna uwekezaji mkubwa wa madini unakuja nchini, hivyo kusema kuwa watashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha wanavutia uwekezaji hususan katika madini ya ‘graphite’ na ‘nickel’.
Aliweka wazi kuwa, kuna baadhi ya taasisi za fedha ambazo zimejitokeza katika sekta ya madini katika nyanja za uchenjuaji, uchimbaji na biashara ya madini.
Profesa Manya alisema kwa sasa sekta ya madini imekuwa ikichangia vyema mapato ya halmashauri, hususan Mgodi wa GGM, ambao unachangia sh. bilioni 10 katika Halmashauri ya Geita.
Alisema wizara yake itasimamia kuhakikisha lengo la serikali katika sekta ya madini kuchangia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, linafikiwa.
Hata hivyo, alisema maonyesho ya sekta ya madini yanaendelea kupanua wigo wa uelewa wa wananchi katika maeneo ya taratibu za biashara na sheria.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema serikali imeweka mitambo mitatu ya kusafisha madini katika mikoa ya Dodoma, Kibaha (Pwani) na Geita.
Dk. Nchemba alisema kuwa mitambo hiyo itakuwa ikisafisha madini kwa asilimia 99, hali itakayosaidia kuokoa fedha za kupeleka kusafishwa nje ya nchi.
Alisema nchi itanufaika kwa kuwa wafanyabiashara wengi watapenda kununua madini nchini kutokana na hali ya usalama uliopo.
Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, alitaka suala la wizi wa rasilimali za nchi lianze kuangaliwa kuanzia ngazi ya familia.
Kanali mstaafu Lubinga, alisema wazazi watakapowafundisha watoto wao maadili mema watakuwa na msingi mzuri wa kimaadili katika taasisi za umma.
Alisema si vizuri kuitupia lawama Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), pekee yake, badala yake malezi yaanzie ngazi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, alisema asilimia 40 ya dhahabu inayochimbwa nchini inatokea Geita, hivyo kusema kuwa wanataka maonyesho hayo kuwa ya kimataifa.
Na SIMON NYALOBI