WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Stergomena Tax, amesema hali ya ulinzi na usalama katika mipaka ya Tanzania yenye urefu wa kilometa 5,461.20 na kuhusisha eneo la nchi kavu na majini, ipo shwari
Mipaka hiyo ni baina ya Tanzania na Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara hiyo katika mwaka wa Fedha 2022/2023, Waziri huyo amesema katika kipindi hicho hapakuwa na matukio ya uhasama yaliyoripotiwa baina Tanzania na nchi zinazopakana, licha ya kuwepo changamoto kadhaa.
MPAKA WA TANZANIA NA DRC
Stergomena alisema hali ya usalama wa mpaka huo ni shwari kwani hakuna tukio la kuhatarisha usalama kwa nchi.
Hata hivyo, alisema ndani ya DRC yameripotiwa matukio ya waasi kushambulia miji mbalimbali nchini humo.
“Wizara kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imeendelea kuwa macho na kujipanga wakati wote. Aidha, ushiriki wa Tanzania katika misheni ya Umoja wa Mataifa (UN) katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (United Nations Organisation Stabilization Mission in the Democratic Republic of the Congo – MONUSCO) unaisaidia nchi kujiimarisha kiulinzi ipasavyo,” alisisitiza.
MPAKA TANZANIA NA MALAWI
Stergomena alieleza kuwa hali ya usalama ya mpaka huo ni shwari na hakuna tukio la kuhatarisha usalama lililoripotiwa.
Alisisitiza kuwa ushirikiano uliopo baina ya Jeshi la Tanzania na Jeshi la Malawi ni mzuri na inajidhihirisha kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo ambayo yamesababisha kufanyika michezo ya kirafiki kati ya timu za majeshi ya nchi hizi mbili yaliyofanyika Brigedi ya Kusini, Julai mwaka jana.
“Changamoto ya mpaka katika Ziwa Nyasa inaendelea kufanyiwa kazi kupitia Tume Maalum ya Usuluhishi (High Level Mediation Team) iliyoundwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Serikali yetu kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kutumia njia za kidiplomasia ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo,” alieleza.
Kuhusu hali ya mpaka wa Tanzania na Zambia, alisema hali ya usalama katika mpaka huo ni shwari na hakuna tukio la kuhatarisha usalama wa nchi lililoripotiwa hadi sasa.
MPAKA TANZANIA NA BURUNDI
Akieleza hali ya usalama wa mpaka huo, alisema hali ni shwari kwani hakuna matukio yoyote yaliyoripotiwa kuhatarisha usalama baina ya nchi hizo, ingawa eneo hilo linakabiliwa na uwepo wa wahamiaji haramu, uvamizi wa wakulima na uingizaji wa mifugo kwa ajili ya kupata malisho ambapo JWTZ imeendelea kukabiliana na hali hiyo.
MPAKA TANZANIA NA RWANDA
Waziri huyo wa ulinzi alisema usalama wa mpaka huo ni shwari, ingawa yapo matukio machache ya kihalifu ya wahamiaji haramu na uingizaji wa mifugo kwa ajili ya malisho. Wizara kupitia JWTZ inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti matukio hayo.
MPAKA TANZANIA NA UGANDA
Stergomena alibainisha kuwa hali ya usalama katika mpaka huo ni shwari na hakuna tukio la kuhatarisha usalama wa nchi.
Hata hivyo, alieleza uwepo wa changamoto ya uingizaji haramu wa mifugo kwa ajili ya malisho.
Alisema juhudi za kuimarisha mpaka zinaendelea kwa kuongeza alama kati ya marundo ya mawe yaliyowekwa na mkoloni, na kujenga barabara ya usalama kwenye Mpaka
MPAKA TANZANIA NA KENYA
Alieleza kuwa hali ya usalama wa mpaka baina ya Tanzania na Kenya ni shwari na hakuna tukio la kuhatarisha usalama dhidi ya Tanzania lililoripotiwa.
Alibainisha kuwa ipo changamoto ya kuharibiwa kwa alama za mpaka na kazi ya kuimarisha mpaka huo inayotekelezwa na timu ya wataalam kutoka Tanzania na Kenya inaendelea vizuri, ambapo awamu ya kwanza imeanzia eneo la Serengeti hadi Ziwa Natron.
MPAKA WA TANZANIA BAHARI YA HINDI
Kuhusu mpaka wa Tanzania katika Bahari ya Hindi, alisema hali yake ni shwari.
Waziri huyo alieleza kuwa katika mpaka huo Tanzania imepakana na nchi za Comoro na Shelisheli.
“Hakuna tukio lililoripotiwa la kuhatarisha usalama dhidi ya Tanzania. Aidha, JWTZ imeendelea kufanya doria za mara kwa mara katika eneo la Bahari ya Hindi ili kubaini na kuzuia wahamiaji haramu, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji wa dawa za kulevya na matishio ya kigaidi,” alibainisha.
MPAKA WA TANZANIA NA MSUMBIJI
Kwa mujibu wa waziri huyo wa ulinzi, alisema hali ya usalama wa mpaka huo ni ya wastani kutokana na mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Ansar Al Sunna Wal Jamaah (AASWJ) maeneo ya Kaskazini mwa Msumbiji, katika Jimbo la Cabo Delgado linalopakana na Mkoa wa Mtwara.
Alisema kundi hilo limekuwa likiathiri usalama kwa kuharibu na kupora mali za wananchi.
“Katikakupambananachangamoto hii, JWTZ imeendelea kuimarisha ulinzi kwa kufanya operesheni za ndani ya nchi kukabiliana na kundi hilo. Aidha, JWTZ inashiriki operesheni chini ya Mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika nchini Msumbiji (SADC Mission in Mozambique – SAMIM) katika jitihada za kudhibiti ugaidi.
Aliongeza kuwa: “Operesheni hizi zimeendelea kuimarisha ulinzi katika eneo la Mpaka, kudumisha amani na utulivu.”
Stergomena alisema operesheni hizo zimesaidia kupunguza nguvu ya kundi hilo la kigaidi, hata hivyo, kundi hilo linatekeleza mashambulizi kwa kuhamahama na kubadili mbinu za kimapigano.
Licha ya hali hiyo, alisema Tanzania inaendelea kupambana kuhakikisha kundi hilo halileti madhara zaidi.
“Wizara inaishukuru Serikali hususani, Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kipaumbele katika kupambana na suala hili, kutoa fedha kwa ajili ya mahitaji mbalimbali yanayosaidia vikundi vya ulinzi kupambana dhidi ya kundi hilo,” alieleza.
Stergomena alisema katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imelenga kutekeleza mpango na bajeti kwa kuzingatia mambo Dira na Dhima ya Wizara, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Aliyataja mambo mengine yatakayozingatiwa katika bejeti hiyo ni Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Alibainisha kuwa katika mwaka huo wa fedha, serikali inatarajia kutenga fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, jumla ya sh. trilioni 2.7 ambapo kati ya fedha hizo, sh. trilioni 2.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. bilioni 230.3 kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.
Na MUSSA YUSUPH, DODOMA