Na FRED ALFRED,Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, amesema mfumo wa Mita za Malipo Kabla ya Matumizi (LUKU) kwa wateja maji unatarajia kuanza mwezi ujao.
Amesema mfumo huo utasaidia kuondoa malalamiko ya wananchi kubambikiwa ankara za maji.
Mhandisi Sanga aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha ushirikiano baina ya Wizara za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zenye dhamana ya sekta ya maji.
“Tunafikiria kuanza kutumia mita za kulipa kabla ya matumizi na sasa tupo katika maandalizi, hivyo tunategemea ndani ya wiki mbili maandalizi yatakuwa yamemalizika na kuanzia Julai tutaanza kufunga rasmi kwa wateja wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Changamoto ambayo kwa sasa tunakumbana nayo ni malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kubambikiziwa ankara za maji, mfumo huu wa kufunga mita za LUKU kabla ya matumizi umependwa na watu wengi kwa sababu mteja atalipa kwanza halafu ndio anapata huduma.”
Mhandisi Sanga alisisitiza kuanza kutenga maeneo kwa ajili ya kuhifadhi maji taka ambapo sasa ni asilimia 30 ya maji taka ndiyo yanayohifadhiwa.
“Itakuwa haina maana yoyote kama nguvu kubwa tutaweka katika maji safi alafu tukasahau namna ya kuhifadhi maji taka, kwa kuwa utafiti unaonyesha kuwa ukipeleka maji asilimia 80 kati ya hizo 40 yatakuwa maji taka,” alifafanua.
Alisisitiza kwamba, suala zima la kutafuta maeneo Tanzania Bara na Zanzibar kwa sababu miradi ya maji safi inahitaji, huku akisema wasipokuwa makini watajenga miradi ya maji safi, lakini wasipoweka mikakati ya kuondoa maji taka itakuwa ni shida.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Madini Zanzibar, Dk. Mngereza Mzee Miraji, alisema ushirikiano katika sekta ya maji miongoni mwa pande zote mbili ni jambo zuri kwa sababu itasaidia kuboresha utendajikazi miongoni mwao.
Alisema ndoto ya ushirikiano ilikuwepo tangu miaka ya 50 iliyopita na sasa imetimia kwa vitendo.
“Wizara ya Maji na Madini kutoka Zanzibar tumepokea kwa mikono miwili suala la ushirikiano wa kisekta na Tanzania Bara, tunaamini ushirikiano huu utazaa matunda kwa wananchi wa pande zote mbili,”alisema.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, alisema sekta ya maji imeendelea kufanya vizuri kutokana na ushirikiano uliopo baina ya viongozi wote katika sekta hiyo.
“Tusisubiri kusifiwa na mtu, ukweli miongoni mwa sekta ambazo zinafanya vizuri hapa Tanzania Bara huwezi kuacha kuongelea sekta ya maji, imekuwa bora sana, tuendelee kushirikiana miongoni mwetu,” alieleza.