BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza orodha ya awamu ya pili ya wanafunzi 7,364 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 19.4 kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru wakati akitangaza orodha hiyo.
Amesema orodha hiyo, imefanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kufikia 45,095 ambao waliopangiwa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 119.3.
Badru amesema tayari wameanza kupeleka fedha za wanafunzi hao waliopangiwa mikopo awamu ya pili katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA, kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.
“Serikali imetupatia fedha, tumeanza kuzipeleka vyuoni… Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa, wanazikuta vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” alisema.
Kuhusu kutangazwa orodha ya awamu ya tatu, Badru alisema wanafunzi waliopangiwa mikopo watatajwa keshokutwa, baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea, akawataka waombaji kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.
“Orodha hii ya pili, inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa na wahitaji, wameomba kwa usahihi na wamekamilisha taratibu za udahili wa chuo.
“Tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine, tutatoa orodha ya tatu katika siku tatu zijazo, yaani Jumatatu Oktoba 25, 2021,” alisema.
Kwa mujibu wa Badru, Serikali imetenga sh. bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 160,000.
Alisema kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.
Badru alisema wamepokea fedha kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na taratibu za malipo zimekamilika na fedha za wanafunzi zilitarajiwa kufika vyuoni kuanzia jana.
Mkurugenzi Mtendaji huyo aliwataka wanafunzi kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.
Na MWANDISHI WETU