MKURUGENZI Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Said Seif, amesema shirika hilo ni lazima linunue mafuta ya karafuu na vitu vitokanavyo na karafuu na siyo ya mimea mengine.
Hayo aliyasema alipozungumzia malalamiko yaliyotolewa na wakulima wa zao la mchaichai, Kisiwani Pemba, kuhusu shirika hilo kushusha bei ya mafuta ya mchaichai, wakati bei ya soko la bidhaa hiyo iko pale pale.
Amewashauri wakulima wa mchaichai, iwapo wanaona kuna sehemu nyingine wanaweza kupata fedha zaidi, wakauza bidhaa zao.
“Sisi tunanunua pale tunapokuwa na uhitaji, huwa tunauza ujazo mdogo katika soko la ndani, siyo la dunia, kwa hiyo mkulima ana hiari yake kwenda kuuza, anajua atapata bei kubwa, hawajakatazwa,”alisema
Alisema mafuta ya mchaichai hayana soko duniani kama yalivyo mengine, jambo ambalo hulisababishia shirika hilo kupata hasara kila mwaka kwa kuwa, wanunuzi wake unasuasua.
“Hiyo bei ya shilingi 300,000 sijui wameipata wapi kwa sababu sisi tunauza katika vichupa, siyo kwa ujazo huo wanaosema wao, hivyo wanayoyasema siyo sahihi hata kidogo,” alisema
Awali, wakiwasilisha malalamiko hayo walipozungumza na gazeti kwa nyakati tofauti, mkulima Khamis Ramadhan Faraji wa kijiji cha Mbiji, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, alisema shirika hilo lilikuwa likiwahamasisha wakulima kulima mchaichai, ingawa kwa sasa wameanza kuvunjika moyo kutokana na bei waliyowekewa.
Faraji alieleza kinachowashangaza ni kuwa, soko la mafuta ya mchaichai halijashuka, lakini wakulima wameshushiwa bei kutoka sh.200, 000 hadi kufikia sh.120,000, jambo ambalo limewatia hasara kubwa.
Mkulima huyo alisema ipo haja kwa ZSTC kuwaangalia kwa jicho la huruma wakulima hao kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi kubwa huku wakiajiri vijana wa kuwasaidia, ingawa kwa sasa wameshindwa kuwalipa wasaidizi.
Alisema katika soko la kimataifa lita moja ya mafuta ya mchaichai wananunua sh.320,000 ingawa shirika linanunua kwao kwa sh.120,000, jambo ambalo linawatia hali unyonge kutokana na kuwa wao ndio wanaofanya kazi kubwa.
Mkulima huyo aliweka bayana kuwa shamba lake lina ukumbwa wa ekari tatu na nusu ambalo huzalisha mafuta mengi baada ya mavuno ila kinachowasikitisha ni wameanza kukata tamaa waliyokuwa nayo kutokana na zao hilo.
Alieleza kuwa kwa sasa kiwanda kilichokuwa kinawasaidia kukamulia mafuta hayo kimeharibika, jambo ambalo linawarejesha nyuma zaidi kiutendaji, hivyo aliiomba serikali kuwatengenezea ili kuondokana na changamoto hiyo.
Naye, mkulima wa zao hilo, Salma Said Rashid wa kijiji cha Chonga, Wilaya ya Chake Chake, alisema wakulima wa zao hilo wamekuwa wakipata hasara kutokana na kushuka kwa bei na kukosekana kwa kiwanda cha kukamulia mafuta hayo.
“Tunapata shida wakati tunapotaka kupeleka mchaichai wetu kiwandani, kwa sababu tukipeleka kiwanda cha Mgelema mhusika mkuu anatuambia kiwanda chake ni cha kukamulia majani ya mkarafuu na siyo mchaichai na kule Mtakata mafuta hayatoki kwa kuwa nyungu zao ni mbovu,”alisema
Alisema awali walikuwa wanapata faida wao na wananchi wengine, kutokana na kuwa wakinunua zao hilo katika maeneo tofauti wanawasaidia kukuza kipato chao, ingawa kwa sasa wanashindwa.
Naye, Asha Juma Rihan, mkulima wa zao hilo anayemiliki shamba lenye ukubwa wa ekari saba lililoko kijiji cha Pujini, alisema hadi kukamilisha upandaji wa zao hilo ametumia takriban sh.milioni mbili.
“Gharama ya ushughulikiaji zao hili ni kubwa sana, mara zote natumia gharama zaidi ya shilingi milioni mbili, lakini napata faida, ila kwa sasa hata gharama tuliyotumia hairudi,” alisema