MLINZI wa Shule ya Winning Sprit inayomilikiwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranqhe, Dinaoh Issa (57), amekutwa ameuawa usiku wa kuamkia Februari 2, 2022, kwa kukatwa na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.
Imedaiwa kuwa watu ambao hawajafahamika waliofanya tukio hilo katika Mtaa wa Olkung’u, ulioko Kata ya Terati, jijini humo, waliondoka na kichwa cha mlinzi huyo.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO), Joshua Mwafilango, akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo, alikiri kutokea tukio hilo.
Amesema mpaka sasa wanamshikilia mlinzi Raymond Mollel, kwa uchunguzi zaidi, ambapo katika uchunguzi wa awali mlinzi huyo amekiri kuhusika na tukio hilo.
“Tunamshikilia huyu mlinzi maana katika eneo hili la shule lina walinzi wawili ambao mmoja ni huyo marehemu na mwingine tunaye, ambaye amekiri tunaendelea na mahojiano kufahamu zaidi chanzo cha mauaji haya,” amesema.
Hata hivyo, alisema baada ya kukagua eneo la mauaji walifanikiwa kupata kichwa cha marehemu na mwili ambao umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa Mount Meru.
Akizungumza tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkung’u, Kata ya Terati, Daud Topiwo amesema Februari 2, asubuhi, aliitwa na wananchi wake kwenda eneo la tukio kuona kiwiliwili cha mlinzi huyo na alipofika alishangaa kuona hakuna kichwa cha marehemu.
“Ni kweli tukio hilo la kinyama limetokea katika mtaa wangu, ambapo asubuhi ya kuamkia leo jana katika eneo la Shule ya Winning Spirt, mlinzi ameuawa kwa kukatwa kichwa kisha waliofanya uhalifu huo kutokomea na kichwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Topiwo, mlinzi huyo analinda eneo hilo kwa miaka mingi na hakuwa mtu wa kugombana na majirani wanaozunguka eneo hilo, kwani muda wote alikuwa anakaa eneo lake la kazi.
Aidha, alisema wao kama wananchi wanaliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wao na utaalamu walionao kubaini wahalifu wa tukio hilo.
“Ila mimi kama kiongozi wa mtaa huu nitaitisha mkutano wa hadhara na wananchi wangu ili tuweke mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo letu,” amesema.
Amewaomba wananchi kutojiingiza katika vitendo hivyo vya kinyama na visivyofaa kwa binadamu, badala yake waelewe Mungu yupo na malipo yapo hapa hapa duniani.
Mmiliki wa eneo hilo, Mstahiki Meya Iranqhe amesema amesikitishwa na kitendo hicho cha kinyama na kukiri marehemu alikuwa mmoja wa wafanyakazi wake.
“Nimesikitika sana mlinzi wangu kuuawa kinyama lakini kwa sasa siwezi kusema lolote, naomba tuwaachie zaidi Jeshi la Polisi lifanye kazi yao,”ameema.
NA LILIAN JOEL, Arusha