NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme, ameagiza uchunguzi dhidi ya watumishi wa afya wilayani Uvinza kuwataka wananchi kuvua viatu wanapoingia wodini kuwatembelea wagonjwa.
Mndeme alisema mtumishi atakayebainika kutoa agizo hilo kinyume cha utaratibu, hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa muhusika.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika Shina Namba 1, Tawi la CCM Nyakatakala A, wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
“Hii ni kero ambayo wakina mama inawasumbua kuwambiwa kuvua viatu wanapoingia wodini.
Wanachohofia wanasema tunavua viatu kuingia wodini inawezekana mule wodini sio salama unaweza ukaondoka na magonjwa mengine.
Aliongeza kuwa: “Nakuagiza kamisaa wetu (Mkuu wa Wilaya) serikali lichunguzeni hili suala la wanawake kulazimishwa kuvua viatu pindi wanapoingia wodini kuwajulia hali wagonjwa.”
Alisema uchunguzi ufanyike kubaini nani aliyetoa maagizo hayo na kwasababu zipi na hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa muhusika.
“Ni mtu mmoja ameamua watu wasiingine na viatu. Ni hospitali gani watu tunaingia bila kuvaa viatu?. Hakuna hospitali ambayo watu wakienda wanavua viatu.
“Kwanini hapa tunaambiwa tuvue viatu? hili limeleta ukakasi. Hawa wahudumu nani kawapa maelekezo ya kuwavua viatu ndugu wa mgonjwa?.
Serikali lichunguzeni kama mtu ameamua kwa mapenzi yake kuwavua watu viatu hatua za kinidhamu zichukuliwe,” alisisitiza huku akishangiliwa na wananchi baada ya kutoa agizo hilo.
Awali, katika risala iliyosomwa na Katibu wa Shina hilo, Ali Kimilila, alisema miongoni mwa changamoto za wananchi wa Kata ya Basanza ni wahudumu wa afya kuwataka kuvua viatu pindi wanapoingia wodini kuwatembelea wagonjwa.
Akielezea kwa undani kuhusu vitendo hivyo, Mkazi wa Kijiji cha Basanza, Neema Julius, alisema imekuwa kawaida kutakiwa kuvua viatu wanapoingia wodini kuwatembelea wagonjwa.
Kutokana na malalamiko hayo, Mndeme alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza kujibu malalamiko hayo mbele ya wananchi katika mkutano huo.
Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Hussein Kateranya, alisema malalamiko hayo ameyasikia kwa mara ya kwanza, hivyo aliahidi kuyafanyia kazi kubaini wahusika na sababu za kutoa agizo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Anafi Msabaha, alisema serikali itachunguza suala hilo na kuchukua hatua kwa wahusika.
NA MUSSA YUSUPH, UVINZA