MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, amemvua madaraka Ofisa Mtendaji wa Kata ya Levolosi, Elisha Emmanuel, kwa kushindwa kuhudhuria mkutano rasmi wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika kata hiyo.
Mongela amefikia uamuzi huo baada ya mfanyabiashara mdogo katika Soko la Kilombero, Mohamed Salum, kumweleza Mkuu huyo wa mkoa kuwa, mtendaji huyo alishiriki njama ya kumnyang’anya kinyemela eneo lake katika soko hilo na kutupa meza yake, kisha kumpa mtu mwingine ajenge kibanda.
Baada ya maelezo hayo, RC Mongela alimwita ofisa mtendaji huyo kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo, lakini hakuwepo eneo la mkutano licha ya mkuu huyo wa mkoa kuambatana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjema, Mkurugenzi wa Jiji Dk. John Pima na wakuu wa Idara wa halmashauri ya Jiji.
Muda mfupi baadaye, mtendaji huyo alifika na alipoulizwa na Mkuu wa mkoa sababu ya kuchelewa mkutano huo, alidai alikwenda hospitali baada ya kujisikia vibaya kiafya, madai ambayo alishindwa kuyathibitisha baada ya kutakiwa kufanya hivyo na RC Mongela.
Na Lilian Joel