MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, amefungua rasmi Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).
Tukio hilo amelifanya kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika viwanja vya maonyesho vya Julius Nyerere, Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Makamu wa Rais amewatahadharisha wazalishaji wa bidhaa hapa nchini kujali ubora na kuepuka ujanja ujanja.
Dk. Mpango amesema ujanja ujanja kwenye biashara unaua biashara kwa sababu kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni rahisi kujua bidhaa iliyo chini ya viwango na ile ilivyokidhi viwango vya ubora.
Hata hivyo, amesema ameridhishwa na viwango vya ubunifu vilivyooneshwa na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali za hapa nchini, ambao wanashiriki katika maonyesho hayo ya mwaka huu yanayotarajiwa kufikia tamati, Julai 13, mwaka huu.