KAMATI ya Uwezeshaji ya Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, mjumbe Albert Chile, amesema wamefanya ziara kwenye mradi huo,Juni 23 na 24,mwaka huu, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ujenzi wake.
Chile amesema hatua iliyofikiwa kwenye mradi huo ni kubwa ikilinganishwa na makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, katika Bonde la Mto Rufiji mkoani Pwani.
Amesema kamati imekuwa ikifuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo, tangu hatua za awali hadi sasa na kwamba kwa maendeleo yake, wana imani mradi huo utakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Mjumbe huyo amesema kamati hiyo imeundwa mahsusi ikihusisha wajumbe kutoka wizara na taasisi mbalimbali za serikali, kwa lengo la kurahisisha na kufuatilia utekelezaji wa mradi kwa kuhakikisha majukumu yote katika makubaliano ya mkataba yanatekelezwa kwa wakati sahihi pamoja na kuishauri serikali.
Kamati hiyo ilitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa mradi huo, ambayo ni handaki la Kuchepusha maji ya mto, kingo za bwawa husika, tuta kuu la bwawa, kituo cha kuchochea umeme na nyumba ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme.
Aidha walitembelea na kukagua Daraja la Kudumu, Barabara, Njia ya kupitisha maji ya kuzalisha umeme na eneo la ufungaji wa mitambo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Christopher Bitesigirwe, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika Juni, mwaka 2022.
Na ZUENA MSUYA