JANGA la Virusi vya Corona (Uviko-19) ni moja ya mambo yaliyoifanya Bohari ya Dawa (MSD), kuja na mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini, hivyo kuboresha utolewaji wa huduma za afya.
Mbali na ugonjwa huo kutazamwa kama tishio duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia MSD imegeuza changamoto hiyo kuwa fursa ya kujitanua katika huduma za afya kwa kujenga viwanda vyake vya kuzalisha vifaa kinga.
Akizungumza wakati wa semina na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Dk. Gabriel Mhidze, amesema hatua hiyo imekuja baada ya uviko-19 kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya dawa na vifaa kinga na tiba nchini.
“Niliwaita wataalamu na kuwaambia tuna tatizo hili la kitaifa na ulimwengu mzima, tunafanyaje? wakaja na mawazo mazuri, tukaanza kutengeneza vitu vyetu sisi wenyewe,” alisema.
Alisema kila mtaalamu katika ofisi hiyo alipeleka wazo la kitu anachotaka kutengeneza kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za huduma wakati wa janga hilo.
“Wakaleta maandiko mengi tukachagua moja linaloweza kutekelezeka kwa haraka, kwa kuwa tusingeweza kutekeleza yote kwa pamoja,” alieleza.
Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba, wote walipendekeza kuanza na andiko la kutengeneza barakoa na changamoto ilibaki juu ya upatikanaji wa mshine kwa ajili ya kufanikisha hilo.
Alisema kwa wakati huo upatikanaji wa mashine hadi ifike nchini ingechukua miezi miwili, hivyo waliamua kuiagiza na kuletwa nchini kwa usafiri wa ndege, ambapo iliingizwa nchini ndani ya wiki moja.
Aliongeza mashine hiyo ya kutengenezea barakoa ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuingia nchini.
Alieleza kwamba kabla ya utengenezaji wa barakoa nchini, bidhaa hiyo ilikuwa ikinunuliwa Afrika Kusini ambako nao waliingiza kutokea China, hivyo kufanya gharama zake kuwa kubwa.
Kwa mujibu wa Meja Jenerali Mhidze, fursa nyingine waliyoitumia kupitia janga hilo ni uzalishaji wa vitakasa mikono, ambapo vilitengenezwa katika ujazo tofauti na kusambazwa kwa watumiaji.
Alisema ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa uwepo wake MSD, taasisi hiyo imefanikiwa kufufua kiwanda cha dawa cha Keko na sasa kinazalisha aina 10 za dawa, huku matarajio yakiwa kuongeza uzalishaiji.
Alitaja viwanda vingine ni pamoja na kile cha kuzalisha mipira ya mikono ambacho kimeshakamilika na Novemba mwaka huu kikitarajiwa kuanza uzalishaji na vingine vitatu vya dawa vyote vikiwa Idofi, Makambako mkoani Njombe.
Na JUMA ISSIHAKA