BOHARI kuu ya Dawa (MSD), imesema imeanza mpango wa usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanisha kwa kishindo ambapo hadi kufikia Oktoba 16 hakutakuwa na kituo cha kutolea huduma nchini chenye uhitaji.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu alilolitoa juzi akiwa Mkoani Tanga, kwa kuipa MSD wiki moja na kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa bohari hiyo, Meja Jenerali Gabriel Mhidze, kuhakikisha hadi kufikia Oktoba 16 mwaka huu, dawa ziwe zimepatikana nchini kote.
Waziri Mkuu alisema maelekezo ya serikali, ni kuwa vituo vyote vya kutolea huduma zikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa lazima ziwe na dawa.
Kutokana na hali hiyo Meja Jenerali Mhidze, amewaeleza waandishi wa habari kuwa mpango wa usambazaji dawa hizo umeanza kwa kishindo na MSD imefanya kufuru kwa kusambaza dawa nyingi ambapo usambazaji wake haujawahi kutokea.
Amesema, kufuatia agizo hilo la Waziri Mkuu utekelezaji umeanza mara moja, ambapo tani 10 na makonteni zaidi ya sita tayari yameshaingia na usambazaji wake umeanza.
Amesisitiza kuwa magari yenye dawa hizo kutoka katika kanda za MSD kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma yatasambaa nchi nzima.
“Wilaya ambazo tayari zimeanza kupokea dawa hizo ni Uvinza DC yenye vituo vya afya 42, ambapo gari ya Scania yenye tani 10, Kigoma MC yenye vituo vya afya 13 gari kubwa ya tani 5.5 na Kigoma DC yenye vituo vya afya 38 Land Cruiser mbili zimeshasili na kushusha dawa,”alisema.
Meja Jenerali Mhidze, ameongeza kuwa katika wilaya ya Kasulu DC vituo vya afya 41, Kasulu TC yenye vituo vya afya 15 na Buhigwe DC yenye vituo vya afya 28 tayari magari matano ikiwemo gari kubwa mbili kila moja yenye kubeba tani 5.5 na Toyota Land Cruiser tatu zimewasilisha dawa.
Alitaja maeneo mengine kuwa ni Lushoto yenye vituo 9, Misenyi na Chato katika vituo vyote vilivyopo, Lindi DC yenye vituo 16 na Hai yenye vituo 24 ambapo magari 13 yameshaondoka na kuwasili katika maeneo hayo, ikiwemo Toyota Land Cruiser 6, gari kubwa ya tani 5.5 zipatazo 3, gari kubwa ya tani 10 na Landcruiser hard top 2 zimeshasambaza dawa katika maeneo hayo.
Alisema mbali na usambazaji huo, shehena nyingine za dawa Tani 12 zitawasili nchini kesho huku Oktoba 16 shehena yenye Tani 12 nyingine zikitarajiwa kuingia na kontena 18 zenye dawa zikiwa zipo katika mpango mkakati wa kuwasili nchini.
Meja Jenerali Mhidze, alisema dawa hizo zipo zitakazowasili nchini kwa kutumia ndege na bahari, lengo likiwa ni kumaliza tatizo la uhaba wa dawa lililojitokeza.
Alisema dawa hizo zinazowasili nchini, zinazingatia taratibu zote za manunuzi na ukaguzi na baada ya taratibu za kitaalamu kukamilika zitawafikia wananchi.
Mkurugenzi huyo, alisisitiza kuwa MSD haina changamoto ya usafiri kutokana na magari mengi yaliyopo, hivyo dawa hizo zinazoendelea kuwasili zitafika kwa wakati ili kumaliza changamoto iliyojitokeza.
Alisema tatizo lililopo lilitokana na mifumo ya ununuzi, hivyo litakwisha na kuwa historia, kwakuwa serikali imedhamilia kuboresha huduma za afya nchini.
Alieleza kuwa usambazaji huo utakuwa wa nchi nzima hata sehemu ambapo hazikuwa na upungufu wa dawa.
“Zipo halmashauri ambazo zilikuwa na uhitaji na pesa zao zilishaingia kwenye mzunguko wa manunuzi kwetu kwa kufanya malipo hizo zitapatiwa dawa kwa haraka kulingana na mahitaji yaliyopo,”alisema.
Pia halamshauri na vituo vya kutolea huduma ambavyo havina pesa alisema watazingatia uhitaji walionao, kwakuwa ni wateja wao hivyo aliwatoa hofu na kuwahakikishia kuwa hakuna kituo cha kutolea huduma kitakachokosa dawa hadi kufikia Oktoba 16 mwaka huu.
Na MARIAM MZIWANDA