MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema nchi haiwezi kuingia gizani kama baadhi ya watu wanavyodai kwa kuwa kinachofanyika hivi sasa ni maboresho na matengenezo ya kawaida kikwemo kituo cha kuzalisha umeme wa gesi cha Songas, kilichoko eneo la Songosongo.
Amesema mgao huo, unaotarajia kuanza kesho, hautakuwa na athari yoyote katika shughuli zinazoendelea nchini huku akiahidi kwamba, hakuna miradi mikubwa ya kimkakati itakayokwama kwa sababu yoyote kwani inaendelea vizuri na wakandarasi wapo kazini.
Msigwa aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Pwani kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita na kusisitiza kwamba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linafanya maboresho ya kawaida, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaongezeka nchini.
“Watu waache kuwajaza wengine maneno ya uzushi, kwani maboresho haya ni ya kawaida na nchi haiwezi kuingia gizani,” alisisitiza.
Msigwa amefafanua kuwa, kutokana na hali ya upungufu wa mvua umesababisha vyanzo vya kuzalishia umeme kupungua, hivyo kusababisha mgao unaotokana na kufanyika kwa maboresho.
“Changamoto hii ni kawaida, hivyo wakati wa maboresho hayo yanayofanyika Songosongo itasaidia hali kurejea kama kawaida na maboresho hayo hayatafanya nchi kuingia gizani,” amesema.
Amewaomba Watanzania kutokuwa na hofu ya hali ya juu kutokana na maboresho hayo, kwa kuwa lengo la TANESCO ni kuhakikisha umeme unapatikana wa kutosha.
“Kuanzia Februari Mosi, mwaka huu kutakuwa na mgao ambao lengo lake ni kuboresha visima vya gesi vilivyopo Songosongo, hivyo wananchi waondoe hofu juu ya hilo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Msigwa amesema ipo miradi mikubwa ya kimkakati Mkoa wa Pwani ikiwemo bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji ambapo ujenzi umefikia asilimia 55, Mradi mwingine ni reli ya kisasa (SGR) uliofikia asilimia 95.
Ameeleza kwamba, serikali inahakikisha miradi inaenda vizuri na haijashindwa kuwalipa wakandarasi na wakandarasi hao wanaendelea kulipwa na kuongeza kuwa hadi sasa fedha zimeshatolewa kwa wakandarasi na kazi inaendelea.
WAMACHINGA
Msingwa amebainisha kwamba, serikali imejipanga kikamilifu kuwapatia fedha za mikopo wafanyabiashara wadogo ili waendeleze shughuli zao.
Pia, amesema serikali itahakikisha taasisi ya Machinga inakuwa kamili na rasmi kwa lengo la kuwapatia machinga na mama lishe mikopo ili waendeleze shughuli zao za kibiashara.
“Serikali ya Awamu ya sita imekuwa haipati usingizi kwa sababu ya ukosefu wa ajira kwa vijana hivyo itahakikisha inatengeneza ajira ili kila kijana afaidike,” amesema.
Msigwa amesema Rais Samia amelibeba suala la machinga katika pochi lake na atahakikisha wanapata mikopo ili waendeleze biashara zao.
Amesisitiza kwamba, Rais anatambua changamoto za vijana kukosa ajira, hivyo taasisi ya machinga itasaidia kwa kiasi kikubwa vijana na wafanyabiashara wadogo kupata kipato kupitia fedha zitakazotolewa na serikali.
Kuhusu umeme, Msigwa amefafanua kuwa, mkoa wa Pwani, mradi wa REA II, vijiji 89 vitafikiwa na kupitia mradi wa Ujazilizi, Sh. bilioni 5.5 zimetengwa, Sh. bilioni 12, pia zimetumika na miradi 96 imekamilika na pato la mkoa limekua na kufikia trilioni 2.728 kwa mwaka 2019 .
Akizungumzia fedha za Uviko 19, Msigwa alisema mkoa wa Pwani ulipelekewa sh. bilioni 16 za ujenzi wa madarasa 422, vituo shikizi vipya 37 na shule mpya za sekondari 11 huku fedha za elimu bila malipo zilipelekewa sh. bilioni tano na kuahidi kwamba serikali inaendelea kuweka mazingira bora katika sekta ya elimu.
Akizungumzia sekta ya viwanda, Msigwa ameupongeza mkoa wa Pwani kwa kuwa ukanda wa viwanda, ambapo hadi sasa una jumla ya viwanda 1,453 kati ya hivyo vikubwa 87, vya kati 177 na vidogo 1,057 na umetenga hekta 53.16 kwa viwanda.
Upande wa dawa, amesema serikali imefikia asilimia 89.5 na imeanzisha maduka ya dawa ili kurahisisha upatikanaji wa dawa.
Msigwa amekemea zahanati na vituo vya afya wilayani Kisarawe na maeneo mengine, vinavyofungwa kabla ya wakati na kuwaonya watumishi wa afya wanaoshindwa kutoa huduma bora kwa wananchi .
Akizungumzia barabara ya Makofia-Mlandizi, Msigwa alieleza, ipo katika utekelezaji na sasa inafanyiwa upembuzi yakinifu hivyo wananchi wavute subira.
MWAMVUA MWINYI na REHEMA MAIGALA