Na ALLAN KITWE, Tabora
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Magharibi, imemtia mbaroni mtumishi wa Kituo cha Afya, Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora, Maila Mdemi, kwa tuhuma za kuuza vitendanishi vya serikali vya kupimia mambukizi ya virusi vya ukimwi katika duka lake la dawa.
Akizungumza na UhuruDigital Meneja wa mamlaka hiyo, Kanda ya Magharibi, Dk. Christopher Migoha, alisema mtumishi huyo alinaswa kupitia maofisa ukaguzi wake waliokuwa katika ukaguzi wa maduka ya dawa wilayani humo.
Alisema maofisa hao walifanya ukaguzi wa kina katika duka la mtumishi huyo, ambapo walikuta vitendanishi hivyo mali ya serikali.
“Mtumishi huyo alipotakiwa kueleza alipovitoa vifaa hivyo hakuwa na jibu la moja kwa moja,” alisema.
Migoha alisema mara kadhaa wamekuwa wakiwaonya wamiliki wa maduka ya dawa na wauzaji wa dawa kuacha kujihusisha katika vitendo vya kuihujumu serikali kwa kuiba vifaa na dawa.
Alitoa wito kwa wamiliki hao kuacha tabia hiyo mara moja kwa kuwa mamlaka hiyo ipo makini muda wote na itaendelea kufanya msako wa mara kwa mara wa kushtukiza.
“Yeyote atakayebainika kujihusisha katika vitendo hivyo, sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kufikishwa mahakamani utaratibu utapokamilika ili iwe fundisho kwa wengine hususan watumishi wa umma wasio waadilifu,” alisisitiza.