Na IRENE MWASOMOLA
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema uchunguzi dhidi ya Shedrack Kapanga (34), anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mama na watoto wake, unaendelea.
Pia amesema watuhumiwa wa wizi wa mafuta bandarini, nao watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Muliro amesema jeshi la polisi linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya serikali kukamilisha upelelezi wa tukio hilo.
Hatua hiyo imekuja siku chache tangu kutokea kwa mauaji ya Emilly Mutaboyerwa na wanawe Daniela na Damita, eneo la Masaki.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda Muliro, alisema mashauri yote mawili yanachunguzwa kwa utulivu na weledi mkubwa.
“Mashauri yote mawili yanahitaji utulivu na weledi mkubwa, watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na wakati wowote baada ya kukamilisha upelelezi watafikishwa mahakani haraka iwezekanavyo,” amesema.
Aidha, Kamanda Murilo amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuendelea na shughuli zao kwa amani kwani hali ya ulinzi na usalama mkoani ni shwari.
Juni 12, mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilimkamata Kapanga ambaye ni msaidizi wa kazi za ndani eneo la Magomeni, akiwa katika harakati za kutoroka baada ya kutokea kwa mauaji Emilly na watoto wake wawili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda Murilo siku hiyo, mtuhumiwa anahusishwa kutenda kosa hilo Juni 9, mwaka huu, baada ya kuwapiga kila mmoja na kitu kizito.
Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro, amesema polisi inaendelea na upelelezi wa kina kuhusu tukio la wizi wa mafuta katika bandari ya Dar es Salaam.
Kuhusu tukio hilo, Juni 14, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kwa kushirikiana na jeshi la polisi, walifanya ziara ya kushtukiza katika mtambo wa kupima mafuta bandarini na kubaini wizi wa mafuta hayo.
Jeshi la polisi liliwashikilia watu 15 wanaotuhumiwa kuhusika na wizi huo uliofanyika kwa njia ya kujiunganishia mabomba kutoka bomba kuu linalosafirisha mafuta wakati wa upakuaji melini kwenda bandarini.