MKAZI wa jijini Mbeya, Robert Edwin (41), amemfikisha mkewe katika Mahakama ya Mwanzo Uyole, akidai talaka kwa madai ya kuchoshwa na tabia ya ulevi ya mkewe ambayo inamfanya kupika ugali na mboga ndani ya sufuria moja.
Akitoa maelezo yake mbele ya Hakimu Nitike Kiputa wa mahakama hiyo, Edwin alidai yeye na mkewe Halima Asajile walifunga ndoa ya kimila miaka kadhaa iliyopita, ambapo hakuwa akinywa pombe.
Alidai baada ya mke wake kujifungua mtoto wa pili, alianza tabia ya ulevi inayomfanya ashindwe kutimiza majukumu yake, ikiwemo kuandaa chakula cha familia.
“Mheshimiwa hakimu huyu mwanamke amekuwa mlevi kupindukia, kitendo kinachompelekea kushindwa hata kupika chakula. Anachanganya vyakula vyote mboga na ugali kwenye sufuria moja,” alidai mahakamani hapo.
Edwin alidai kitendo hicho kimekuwa kikimshangaza, kwani siku ya kwanza ambayo mkewe alichanganya mboga ya majani, mchele, nyanya na kitunguu ndani ya sufuria moja, alidhani mke wake amebadilisha mtindo wa mapishi.
“Mheshimiwa hakimu siku ya kwanza nilishindwa kumuuliza nikajua labda ameamua kunibadilishia mapishi ila baada ya kunichanganyia tena unga wa ugali, dagaa, nyanya na vitunguu kwa pamoja ndipo nilipogundua alikuwa amelewa.
“Kwa hatua iliyofikia ninachokitaka hapa ni talaka na si vinginenyo, haiwezekani mimi niache pesa ya chakula halafu aende kunywea pombe,” alidai mbele ya hakimu.
Hata hivyo, mlalamikiwa alipoulizwa madai hayo kama ni kweli, alikiri yana ukweli na kusisitiza bado anampenda mumewe na hayupo tayari kuachana naye.
Hakimu Kiputa aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 9, mwaka huu mdaiwa atakapotoa ushahidi wake.
Na ZAWADI KAPAMBWE, Mbeya