MKAZI wa Buswelu wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, Salha Salum (26), anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mumewe sehemu mbalimbali za mwili.
Tukio hilo lilitokea Mei 28, 2022, saa 2:30 usiku, nyumbani kwa wanandoa hao eneo la Buswelu katika Manispaa ya Ilemela mkoani humo huku chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa wivu wa mapenzi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gidion Msuya, alisema mwanaume mmoja jina halijafahamika anadaiwa kumuua mkewe kwa kummiminia risasi zaidi ya moja mwilini na kusababisha kifo chake papo hapo.
Msuya alisema baada ya mauaji hayo mwanaume huyo alitoroka na kukimbilia kusikojulikana na wanaendelea kumtafuta kwa tuhuma hizo za mauaji ya mkewe.
“Tukio hilo lipo, linahusisha wanandoa wawili (mke na mume), mtuhumiwa anatafutwa baada kutoroka na tunachunguza chanzo cha mauaji, ingawa taarifa za awali zinaeleza kuwa ni wivu wa mapenzi,” alisema.
Kaimu Kamanda huyo, alisema mtuhumiwa ambaye hajafahamika jina alitekeleza mauaji hayo kwa kutumia silaha yake aliyokuwa akiimiliki kihalali, lakini aina haijafahamika licha ya maganda kadhaa ya risasi kuokotwa eneo la tukio.
Msuya alisema wanafuatilia silaha hiyo iliyotumika katika mauaji hayo ili kujua ni aina gani. Kwa mujibu wa Msuya, wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo pamoja na kumtafuta mtuhumiwa wa mauaji hayo ili afikishwe katika vyombo vya sheria.
Habari kutoka eneo la tukio, zinadai Salha alifunga ndoa na mumewe huyo mapema mwaka huu kabla ya mfungo wa Mwezi wa Ramadhani.
Inadaiwa mauaji hayo yalifanyika baada ya kumalizika kwa mechi ya Yanga na Simba, marehemu akitajwa kuwa shabiki wa timu ya Yanga na mumewe alikuwa Wekundu wa Msimbazi Inaelezwa kuwa wanandoa hao walishuhudia mchezo huo juzi wakiwa maeneo tofauti katika Uwanja wa CCM Kirumba ambapo Simba ilichapwa goli 1-0.
BALTAZAR MASHAKA, MWANZA