MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu mume, mkewe na wengine sita, kulipa fidia ya sh. milioni 20, baada kutiwa hatiani kwa kosa la kughushi fedha bandia za nchi mbalimbali zikiwemo Marekani na Malawi.
Pia imeamuru kutaifisha gari aina ya Suzuki Carry, pikipiki na vifaa walivyokutwa vinavyotumika kutengeneza fedha bandia, vikiwemo kompyuta aina ya Dell, printer na vibao vinane vilivyochorwa vichwa vya marais wa nchi mbalimbali.
Waliohukumiwa ni Masumbuko Kiyogoma na mkewe Mwanaisha Mtwenge, Epimark Munish, Adamu Lugoza , Malamla Rajab, Elias Wandiba, Ramadhan Twaha na Joseph Ndia.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ritta Tarimo, baada ya washitakiwa hao kuandika barua ya kukiri makosa na kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), kulipa sh. milioni 20 na Fedha hizo zimeshalipwa.
Aidha, Hakimu Ritta aliwahukumu washitakiwa kifungo cha nje mwaka mmoja wasifanye kosa kwa kipindi hicho.
Awali, Wakili wa Serikali Faraja Ngukah, alidai shauri lilipelekwa kwa kutajwa na upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, lakini anaitaarifu Mahakama kuwa washitakiwa wameonyesha nia ya kuingia makubaliano na DPP.
Ngukah alidai kwa kuonyesha nia ya makubaliano hayo na DPP, hivyo alitoa kibali cha kuendesha kesi hiyo ya uhujumu uchumi katika mahakama hiyo na kufanya majadiliano na washitakiwa hao.
Alidai baada ya kufanya majadiliano, washitakiwa walipunguziwa mashitaka yao na kubaki na shtaka moja la kughushi noti za benki, hivyo aliomba mahakama kuwasomea washitakiwa hati mpya ya mashitaka.
Wakili Ngukah, alidai kati ya Januari Mosi 2019 na Februari 29, 2020 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Pwani na Mbeya, washitakiwa walikutwa na fedha bandia na vifaa vya kutengeneza fedha bandia.
Wakili Ngukah alitaja baadhi ya fedha hizo bandia na vifaa vilivyokuwa vinatumika kutengeneza, alidai katika fedha za Tanzania walikutwa na noti bandia za sh. 2,000 zikiwa 497.
Noti za sh.5,000 zilikuwa 610, 10,000 zilikuwa 815 na dola za Marekani 100 zikiwa 815 na dola nyingine 500 zilikiwa 48.
Aliendelea kutaja fedha zingine za Msumbiji noti za sh. 1,000 zikiwa 487 na noti 500 zikiwa 324.
Katika fedha za nchini Congo noti za sh. 1,000 zilikuwa 213, zingine 5,000 zilikuwa 146 na Malawi noti za 500 ilikuwa ni moja na nchini Kenya zilikamatwa noti za sh. 200 moja.
Vile vile alitaja vifaa ambavyo walikutwa navyo kuwa ni Kompyuta mpakato aina ya Dell, printer sita , mashine ya kukatia karatasi moja, simu aina mbalimbali, moderm frash, hot fail grinder na vibao nane vyenye picha za marais.
Ngukah alidai baada ya kukamatwa fedha hizo bandia zilipelekwa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) kwa ajili ya kuthibitisha kama ni bandia.
Wakili Ngukah, baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo na washitakiwa kukiri, Hakimu Ritta aliwatia hatiani kwa kosa la kughushi.
Kabla ya Hakimu Ritta kutoa adhabu, Wakili Ngukah, alidai hana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washitakiwa, lakini makosa waliyokutwa nayo yanagusa uchumi wa nchi, hivyo mahakama itoe adhabu inayostahili.
Alidai Desemba 2, mwaka huu washitakiwa walishalipa sh. milioni 20 ikiwa ni sehemu ya hasara waliyoipatia Serikali kulingana na Makosa yao.
Na SYLVIA SEBASTIAN