MWALIMU wa Shule ya Msingi Radienya Shirati, Kata ya Mkoma, Tarafa ya Nyancha, wilayani Rorya, mkoani Mara, Wilfred Oliech (48), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15.
Akisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Visensia Balyaruha, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Bukulu Bukombe, alidai mshitakiwa alimbaka mtoto huyo (jina limehifadhiwa), Machi na Juni, mwaka huu, kwa nyakati tofauti na kumsababishia maumivu na madhara mwilini.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri kuahirishwa hadi tarehe nyingine y kutajwa.
Hakimu Balyahura alisema kosa la ubakaji lina dhamana. Hata hivyo, mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo alirudishwa mahabusu hadi Agosti 16, mwaka huu, kesi itakapopelekwa kwa kutajwa.
Na Samson Chacha, Tarime