POLISI Mkoa wa Kusini Pemba, imethibitisha kumshikilia mwalimu mstaafu Mohamed Kassim (60), kwa tuhuma za kumpatia ujauzito mtoto mwenye ulemavu wa akili.
Akizungumza na UhuruOnline kwa njia ya simu, mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi, mkoani humo, Richard Tadei Mchomvu, alisema mtuhumiwa huyo anashikiliwa katika kituo cha Polisi Kengeja, Wilaya ya Mkoani.
“Ni kweli mtuhumiwa huyo anaendelea kushikiliwa kituo cha Polisi Kengeja,” alisema.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo ni familia moja na mtoto huyo na kwamba, alikamatwa wiki iliyopita kwa lengo la kuisaidia polisi kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Kamanda huyo alisema mtuhumiwa alikamatwa ili ahojiwe baada ya kutokea kwa tukio hilo.
“Jeshi la Polisi baada ya kupata tarifa zozote za kihalifu, ziwe za ubakaji, wizi au utoroshaji, huwakamata wanaotuhumiwa ili wahojiwe zaidi.
“Ni kweli mtuhumiwa huyo Mohamed Kassim, mwenye umri wa miaka 60, anaendelea kuhojiwa na hatua hiyo itakapokamilika, atafikishwa katika mamlaka nyingine kwa hatua za kisheria,” alisema.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati mtuhumiwa huyo akishikiliwa na
kuhojiwa kwa tuhuma zinazomkabili.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Kengeja, Mohamed Kassim Mohamed, alikiri kutokea kwa tukio
hilo la mtuhumiwa kumpatia ujauzito mtoto huyo mwenye ulemavu wa akili, mwenye umri wa miaka 17.
Alisema alipokea taarifa hizo kutoka kwa Mratibu wake wa wanawake na watoto wa shehia na kisha kutoa taarifa kituo cha polisi kwa hatua nyingine.
“Ni kweli ndani ya moja ya vijiji vilivyomo ndani ya shehia yangu, kuna mtoto mwenye ulemavu amepewa
ujauzito na mwalimu mmoja mstaafu na sasa yupo kituo cha polisi Kengeja,” alisema
HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMED