POLISI Mkoani Morogoro inamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkuyuni, Tarafa ya Mkuyuni, Wilaya ya Morogoro, Musa Hasira (46) kwa tuhuma za kumshambulia hadi kumng’oa jino mwalimu mwenzake Witness Makoti (31), wakazi wa Mkuyuni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu, alisema tukio hilo, lilitokea Oktoba 15, mwaka huu, saa sita mchana maeneo ya Mkuyuni.
Muslimu alisema mwalimu mkuu huyo, alimshambulia mwalimu mwenzake kwa kutumia fimbo, ngumi na kumpiga makofi katika sehemu mbalimbali za mwili.
Kamanda huyo alisema Witness, alipiga kelele za kuomba msaada hadi mwalimu mwingine alipofika kumsaidia.
Alisema chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa na mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa zaidi ambapo Witness, tayari amepatiwa matibabu katika Zahanati ya Mkuyuni.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mkuyuni, Mwinyi Shaabani,alisema mwalimu Witness alikuwa darasani na wanafunzi watatu wa kike wakijadiliana masomo, ghafla alipofika mwalimu mkuu huyo alianza kumshambulia.
Diwani huyo alisema baada ya shambulio hilo na kuokolewa kwa Witness,mmoja wa walimu aliyeshuhudia walienda Kituo cha Polisi Mkuyuni na kupewa PF3 ili akatibiwa katika Zahanati ya Mkuyuni na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Nunge.
Alisema Mwalimu Witness kwa sasa amekuwa akihofia usalama wa maisha yake kwamba, mtuhumiwa akiachiwa, anaweza kumdhuru na aliiomba serikali na jamii anapofanyia kazi kumsaidia ili haki itendeke.
Diwani huyo, alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, viongozi mbalimbali wa wilaya, tarafa na kata wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara.
Alisema kumekuwepo na malalamiko yakitolewa kutoka kwa wanafunzi na baadhi ya walimu kuwa, mwalimu huyo mkuu, amekuwa na tabia zisizoeleweka kwa wanafunzi wa kike na taarifa zinapotolewa, hakuna hatua zinazochukuliwa.
Katika tukio lingine, Kamanda Muslimu alisema katika operesheni mbalimbali mkoani Morogoro, wanawashikilia raia wawili wa Somalia na Ethiopia kwa kuingia nchini bila vibali.
Alisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Maguha wilayani Kilosa ambapo raia hao, walikuwa wakisafirishwa kwa njia ya pikipiki,waliingia nchini wakitokea Somalia kupitia Uganda na walikuwa wakielekea Afrika kusini.
Na LATIFA GANZEL, MOROGORO