POLISI Mkoa wa Lindi, inamtafuta Juma Salumu maarufu Juma Kipanya ambaye ni mganga wa kienyeji kwa tuhuma za kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 15 wilayani Lindi.
Akizungumza na UHURU, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Foka Dinya, amesema mama mzazi wa mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) aligundua kuwa mtoto wake ana ujauzito Desemba, mwaka jana ndipo alitoa taarifa polisi Februari 3, mwaka huu.
Kaimu kamanda huyo alisema wakati taarifa hiyo inatolewa na mama wa mtoto, mtuhumiwa alikuwa ametoroka.
Akielezea tukio hilo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo alidai Juni, mwaka jana, mtoto wake alipelekwa kwa mganga wa kienyeji na babu yake kwa madai ya kwenda kutengeneza dawa, baada ya mganga kutoa sharti kuwa dawa yake lazima itengenezwe na binti kigoli.
Mama huyo alidai mtoto wake alipopelekwa mganga alimbaka na kumtisha asizungumze kwa watu, kwani akisema mizimu itampa adhabu.
Alidai mwanafunzi huyo aliporudi nyumbani hakusema chochote na aliendelea na masomo hadi ilipofika Desemba, mwaka jana, ambapo waligundua hali isiyokuwa ya kawaida na walipombana aliwaeleza alibakwa na mganga huyo alipokwenda kutengeneza dawa ya babu yake.
Na Sophia Nyalusi, Lindi