MWANAFUNZI bora kitaifa katika matokeo ya darasa la saba, Eluleki Haule wa Shule ya St. Anne Marie Academy, amesema ndoto yake ni kuwa mpelelezi na kufanya kazi Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Akizungumza na UhuruOnline mjini Bagamoyo anakosoma masomo ya kujiunga na kidato cha kwanza Shule ya Marian Boys, Haule alisema amekuwa na ndoto ya kuwa mpelelezi kwa muda mrefu.
Alisema awali ndoto yake ilikuwa kuja kuwa rubani wa ndege kubwa, lakini aliibadili na kwa sasa hamu yake kubwa ni kufanya kazi ya upelelezi.
“Awali nilikuwa natamani sana kufanya kazi ya urubani na kwa kweli ilikuwa shauku yangu ya muda mrefu, lakini hivi karibuni nimeona nibadili sasa natamani kuwa mpelelezi tu,” alisema Eluleki ambaye alisema atasomea masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati.
Alisema siri ya ufaulu wake ni kuwa makini darasani, kufanya mapitio ya masomo mara kwa mara, nidhamu na kujituma katika masomo na kumcha Mwenyezi Mungu wakati wote.
Aliwapongeza walimu wa St. Anne Marie Academy kutokana na kutambua wajibu wao kwa kuwa wamekuwa wakiwapa mitihani na mazoezi mengi hali iliyowaimarisha kitaaluma.
Mama mzazi wa Haule, Digna Mlengule alieleza kuwa siri ya mtoto wake kuwa namba moja kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu ni juhudi zake binafsi na walimu wa shule ya St. Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri, Dar es Salaam.
Digna alieleza kuwa Haule ambaye ni mtoto wa kwanza na wa pekee kwa sasa alikuwa na bidiii sana ya masomo na hakuhitaji kusukumwa ili kujisomea wakati wote.
Alisema Haule ni mtulivu, anayejitambua na kufanya mambo yake kwa mpangilio na wala hashinikizwi kutimiza wajibu wake katika masomo.
“Katika suala la masomo hakunisumbua hata kidogo, nakumbuka wakati anaanza ‘pre unit’ tu hapo St. Anne Marie ndipo alikuwa anasumbua ila kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba amekuwa mtu anayejua afanye nini bila kusukumwa.”
“Nawashukuru sana walimu wa St. Anne Marie Acedemy maana amesoma pale miaka yote 10 kuanzia chekechea, wamenipa faraja kubwa sana nawapongeza walimu kwa jitihada zao,” alisema
Kuhusu kazi anayotaka kufanya baada ya masomo yake, Digna alisema mara kadhaa amewahi kumsikia akisema anataka kufanya kazi ya kurusha ndege au kuwa mpelelezi katika idara nyeti.
Digna alisema kwa sasa Haule anasoma masomo ya kuingia kidato cha kwanza Shule ya Marian Boys ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani ila atajadiliana na baba yake ili waone kama aendelee shule hiyo au wampeleke shule nyingine.
Na Mwandishi Wetu