WATU sita akiwemo Lucy Mwaipopo, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma tofauti ikiwemo wizi wa vyuma vya daraja jipya la JPM linalojengwa Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria.
Habari zilizopatikana jijini Mwanza na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mwanza, Ramadhan Ng’anzi zilisema gari moja roli (hakulitaja) na watu watano akiwemo mnunuzi wa vyuma chakavu wa mjini Sengerema, wanashikiliwa na jeshi hilo wilayani Sengerema.
Habari hizo zilisema, Lucy anashikiliwa kituo cha kati jijini Mwanza kwa tuhuma za kujifanya ofisa usalama na kutapeli mamilioni ya watu mbalimbali maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Dar es Salaam, Morogoro na Sumbawanga.
“Kweli matukio hayo yapo, huyo mwanamke Lucy Mbutolwe Mwaipopo leo (jana) ni siku ya nne au ya tano tunamshikilia kwa tuhuma za utapeli na kujifanya ofisa wa serikali, tunaendelea kumuhoji kutokana na kudaiwa kuhusika na vitendo hivyo katika maeneo mbalimbali,” amesema Kamanda Ng’anzi.
Amesema Lucy alikamatwa Mei 17 saa 2:30 asubuhi Mtaa wa Kisasa mkoani Dodoma akiwa na nyaraka za watu mbalimbali aliokuwa akiwadanganya atawasaidia matatizo yao.
Mtuhumiwa huyo pia alikutwa na nyaraka za mashirika mbalimbali wakati akiondoka nyumbani kwake mtaani humo.
Kukamatwa kwake kumekuja baada ya watu zaidi ya 60 wakazi wa Mwanza akiwemo Lazaro Magera kulalamika kutapeliwa zaidi ya sh. milioni 17, walizochanga Aprili, mwaka jana kwa madai anakwenda kushughulikia migogoro yao ya ardhi.
“Tunaishukuru polisi kwa ushirikiano mzuri waliotupatia, karibu watu 60 tukiwemo 14 wenye migogoro ya viwanja Lock City Mall tumetapeliwa zaidi ya sh. milioni 17 tulizochanga akidai ni ofisa usalama,” alisema Jackson Mbeto.
Kuhusu watuhumiwa wa Daraja la JPM Kigongo-Busisi, Kamanda Ng’anzi amesema wanawashikilia watu watano, akiwemo mnunuzi wa vyuma chakavu wa Nyatukara, Sengerema na msako dhidi ya wahusika wengine unaendelea.
NA PETER KATULANDA, Mwanza