MWENYEKITI wa Kitongoji cha Kanami, kilichopo katika Kijiji cha Isangijo, Kata ya Bukandwe, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza, Robert Mfungo, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Habari zilizopatikana jijini mwanza kutoka kijijini humo na kuthibitishwa na polisi, zimesema Mfungo anadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 2, mwaka huu, katika kitongoji hicho.
Kwa mujibu wa habari hizo, mtoto huyo anasoma darasa la sita katika shule iliyoko wilayani humo.
Mkazi wa kitongoji hicho, Hadija Nchola, alidai mtuhumiwa huyo alitenda kitendo hicho usiku.
Diwani wa Kata ya Bukandwe, Mathias Minze alidai baada ya mtoto huyo kutendewa kitendo hicho, alikimbilia nyumba jirani (hakuitaja) ambapo walitoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji na kuijulisha polisi kabla ya kumpeleka kituo cha afya Kisesa.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi, alisema Mfungo aliyekuwa akishikiliwa katika kituo cha Kisesa baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia juzi (Agosti 3), amehamishiwa katika kituo cha Mjini Kati jijini Mwanza.
“Ni kweli tunamshikilia Mwenyekiti wa kitongoji cha Kanami kilichopo Kijiji cha Isangijo wilaya ya Magu, Robert Mfungo kwa tuhuma za kumdhalilisha kijinsia kwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12,” alisema Kamanda huyo.
Ng’anzi alisema uchunguzi wa tuhuma za mwenyekiti huyo kumdhalilisha kijinsia mwanafunzi huyo unaendelea na hatua zaidi dhidi yake zitachukuliwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za Wanawake na Wasichana la KIVULINI, jijini Mwanza, Yassin Ally, amesema tukio hilo lisilokubalika katika jamii, limeligusa shirika lake, hivyo anaomba jeshi la polisi liharakishe uchunguzi na kuchukua hatua stahiki haraka.
Na PETER KATULANDA, MAGU