WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za Uviko-19, ambazo kwa sasa zimeanza kutumika katika kutekeleza miradi miradi mbalimbali hapa nchini.
Aidha, ameelekeza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (IAG) na wakaguzi wote walioko katika ofisi zinazotekeleza miradi kwa fedha hizo kuanza ukaguzi mara moja na kwa wakati kadri utekelezaji unavyoendelea ili kuhakikisa fedha hizo zinatumika katika masuala yaliyokusudiwa.
Akizungumza jijini Arusha kwa niaba ya Waziri Mwigulu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, katika mkutano wa mwaka wa wakaguzi wa ndani kutoka taasisi 486 za ukaguzi, alisema IAG na wakaguzi wote ni vyema kutumia dhana ya ‘Real-time Audit’ katika ukaguzi wa miradi ya ujenzi na manunuzi ya vifaa ili kuhakikisha ubora na thamani ya fedha katika miradi husika.
“CAG utoe mwongozo wa jinsi ya kukagua fedha za miradi ya Uviko-19 haraka, kupitia mkutano huu naomba kuwaelekeza maofisa masuhuli wote wanaohusika katika utekelezaji wa mpango wa kupambana na ugonjwa huo wahakikishe wanatekeleza miradi hiyo kwa uharaka, ubora, tija na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa,” alisema.
Aidha, aliwataka kuzingatia misingi mikuu ya ukaguzi yaani ‘Core principles of Internal Auditing’ ikiwemo uadilifu na weledi wakati wote wanapokuwa katika kazi zao za ukaguzi.
Alisema ni vyema kufanya kaguzi zao kwa kuzingatia viwango na kutoa taarifa sahihi kwa kile walichokiona wakati wanakagua ili kazi zao ziwe na ubora, ziaminike na kuboresha mifumo ya udhibiti wa serikali.
“Pale mtakapopata mashinikizo yasiyofaa katika kutekeleza kazi zenu itumieni Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (OIAG) na kama mtapewa kazi ambazo hamna ujuzi nazo, taratibu mnazijua zikiwemo kufanya kazi na mwenye ujuzi wa kazi hiyo au kumpa afanye kazi hiyo mwenye ujuzi wa kazi husika,” alisema.
Kuhusu changamoto ya uhaba wa wakaguzi wa ndani, serikali italiangalia kwa kina kwa kuhakikisha bajeti mahsusi inatengwa ili wakaguzi wapya waajiriwe.
Kwa mujibu wa Mwigulu, wakati wa sasa unahitaji zaidi ukaguzi wa mifumo, hivyo serikali kupitia wizara Wakala, Idara, zinazojitegemea na mashirika ya umma itaandaa utaratibu wa kuajiri wakaguzi wa mifumo na itasomesha wakaguzi katika fani hiyo.
Aliwasihi wakaguzi kufanya mitihani ya fani mahsus ikiwemo mitihani ya mifumo (CISA) ili kubaki kwenye tasnia ya ukaguzi na kuongeza thamani kutoka kwenye ukaguzi wao kwa ajili ya kuepuka kutupwa nje ya ukaguzi kutokana na kasi ya mabadiliko.
Alisema serikali itagharamia wakaguzi wote wanaotaka kufanya mitihani ya CISA kwa wale wenye sifa na watakaokidhi vigezo vitakavyowekwa ili kuhakikisha mifumo ya kielekroniki inakaguliwa ipasavyo inaimarishwa na kufikia malengo ya uanzishwaji wake kupitia ukaguzi wa mifumo.
“Nakuelekeza IAG kuanza sasa kuandaa mwongozo wa mafunzo ya CISA kwa nchi nzima na pili utenge fungu la kutosha kwenye bajeti yako kwa ajili ya kusomesha wakaguzi katika fani hii ili ukague ipasavyo mifumo ya kielekroniki ya serikali,” alisema.
Naye, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Athumani Mbuttuka, alisema tasnia hiyo pamoja na kuwa muhimu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo idadi ndogo ya wakaguzi wa ndani ikilinganishwa na uzito na ukubwa wa majukumu wanayotekeleza.
“Hadi sasa tathimini iliyofanyika imebaini ikama inataka uwepo wa wakaguzi 2,409 kwa Serikali Kuu,Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma lakini serikali yote ina wakaguzi 1,461 ikiwa ni upungufu wa wakaguzi wa ndani 948 sawa na asilimia 39,” alisema.
Aliongeza: “Hali ya halmashauri zetu mbaya kwani kuna wastani wa wakaguzi wawili kwa kila halmashauri ukilinganisha na wizara ambazo zinawastani wa wakaguzi watano kwa kila wizara, hivyo kunahitajika hatua za haraka katika eneo hili,” alisema.
Hivyo, alisema ukiachilia mbali uhaba wa wakaguzi pia vitengo vya ukaguzi wa ndani vinakabiliwa na ufinyu wa bajeti, uhaba wa vitendea kazi pamoja na kukosekana kwa mafunzo ya kutosha kwa wakaguzi wa ndani.
Na LILIAN JOEL, Arusha