Na WILLIAM SHECHAMBO
MWILI wa aliyekuwa Rais wa tano wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli, usiku wa leo Machi 23, unahifadhiwa katika Ikulu ya Zanzibar, kabla ya safari ya kwenda Mwanza, mapema kesho.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa taarifa hiyo leo, wakati akihutubia maelfu ya wananchi waliofika katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kumuaga mpendwa wao.
Amesema mwili wa Hayati Dk. Magufuli utalala Ikulu Zanzibar na kesho asubuhi mwili utasafirishwa kwa ndege maalumu kwenda jijini Mwanza, kuagwa na wananchi wa mkoa huo na maeneo jirani.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waendelee kutoa pole kwa mke wa marehemu, Mama Janet Magufuli, ambaye hakuweka kufika uwanjani hao na badala yake ametangulia Mwanza.
“Mpaka jana jioni (Machi 22), tunazo taarifa watu waliofuatilia tukio la kuaga kitaifa jana Dodoma mwili wa Hayati Dkt. John Magufuli ni watu karibu bilioni 4, walikuwa wanafuatilia tukio la kuaga kwa mpendwa wetu,” amesema.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, kutoka Mwanza, mwili utasafirishwa kwenda Chato, Geita kwa njia ya barabara kupitia daraja la Kigongo- Busisi na kisha kusimama kwa dakika 10 nyumbani kwa wazazi wa Mama Janet, mjane wa Dk. Magufuli.