BAADA ya kufanya vizuri katika michezo mitano ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kujizolea pointi 15 ikiwa kileleni mwa msimamo, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema hajaridhika kiwango cha kikosi chake kinavyocheza licha ya kupata ushindi mechi zote.
Yanga ilianza vyema katika msimu huu ambapo imeweka rekodi ya kushinda mechi tano za mwanzo katika Ligi Kuu Bara kitu ambacho timu zingine zimeshindwa kufanya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nabi alisema anahitaji kuongeza ufanisi zaidi ili kufikia pale anapopataka, kwani ametumia muda mwingi kukijenga kikosi chake.
Alisema wachezaji wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi ambazo wanashindwa kuzitumia, hivyo anapaswa kulifanyia kazi suala hilo kwani anahitaji kufunga mabao mengi zaidi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa mapema.
“Bado sijaridhika kwa namna kikosi changu kinavyocheza licha ya kupata matokeo maziri katika kila mchezo ambao tumeshuka dimbani, tunahitaji kuongeza ufanisi zaidi ili tufikie pale tunapopataka.
“Tunashukuru tunapata matokeo mazuri, najua Yanga ni timu kubwa Afrika, wakati nimefika hapa nilihitaji muda kidogo kukisoma kikosi na tayari nimefanikiwa kwa asilimia kubwa, hivyo yamebaki mapungufu madogo yakurekebisha,” alisema Nabi.
Alisema anawaomba mashabiki na wapenzi wa timu yake kuendelea kuwapa sapoti ili kuhakikisha wanaendeleza rekodi ya kupata ushindi katika mechi zitakazofuata.
Kocha huyo raia wa Tunisia, alisema anahitaji kutwaa ubingwa msimu huu, hivyo ni lazima wapambane kupata pointi tatu katika kila mchezo na ili kulifanikisha hilo, ni lazima tufanye maboresho katika mapungufu yote ambayo yalijitokeza katika mechi zilizopita.
Yanga walianza ligi kwa kuichapa Kagera Sugara bao 1-0, wakaichabanga bao 1-0 Geita Gold, wakashinda mabao 2-0 dhidi ya KMC, wakashinda mabao 2-0 dhidi ya Azam FC kabla ya juzi kuwashishia kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-1.
Na NASRA KITANA