WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amewataka wakuu wa mikoa yote 31 nchini, kufanya uhakiki wa takwimu za operesheni ya Anwani za Makazi, hasa kipengele cha usimikaji wa miundombinu ya nguzo zenye majina ya barabara, mitaa na namba za nyumba.
Akizungumza katika kikao kazi na wakuu wa mikoa kilichofanyika Jijini Dodoma, Nape alisema uhakiki huo ni muhimu kwa kuwa takwimu za usimikaji wa miundombinu hiyo zinaonyesha zipo chini ukilinganisha na uhalisia wa kilichotekelezeka katika mikoa waliyopita kukagua na kuridhika na utekelezaji.
Alisema ifikapo Mei 27, mwaka huu Wizara hiyo, itakuwa imepeleka fedha katika mikoa yote kufanya uhakiki na kuweka takwimu sawa kulingana na uhalisia, ili taarifa itakayowasilishwa ikiwa imesainiwa na mkuu wa mkoa husika iwe sahihi na itakabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ukiangalia hali ya takwimu, kwa mfano mkoa wa Lindi inaonekana ni asilimia mbili tu ya physical signs ndio imetekelezwa, lakini uhalisia haupo hivyo kwa kuwa nimepita mikoa mingi hadi Zanzibar, nimejionea lakini bado takwimu zinaleta utata, hivyo niwaombeni sana twendeni tukahakiki ili sisi na nyie tuzungumze lugha moja kwa kupata takwimu halisi,”alisema.
Aliongeza kuwa: “Anwani za Makazi zimethibitisha uwepo wa Serikali za Mitaa zilizo imara na zinazomwakilisha vizuri Rais wetu, kama mtu ana mashaka na uimara wenu wakuu wa mikoa miye nitakuwa balozi wenu kwasababu nimepita katika mikoa nimekagua na nimeridhika, lakini pia ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI wamepita kukagua na wamejionea mmefanya kazi nzuri sana.”
Pia, Nape alitumia kikao hicho kupenyeza ajenda ya Wizara anayoisimamia ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali na kuwa imejipanga kufanya semina kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, aliwataka wakuu wa mikoa, kusimamia kanuni za utekelezaji wa Anwani za Makazi ambazo ndiyo msingi wa utekelezaji wa mchakato huo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Jim Yonazi, alisema mchakato wa utambuzi wa makazi ya watu, ni moja ya eneo muhimu litakalosaidia nchi kuingia katika uchumi wa kidijitali unaoruhusu wananchi kujihusisha na shughuli za kiuchumi mahali walipo.
“Niwashukuru sana wakuu wa mikoa kwa kufanya kazi hii kwa kiwango cha juu na ufanisi mkubwa ambapo sasa tumefikia asilimia 106.62 ya utambuzi wa makazi, asilimia hizi zimedhihirisha kuna makazi tuliyokuwa hatuyatambui awali na kupitia zoezi hili tumeyatambua na yatajumuishwa kwenye mipango ya maendeleo,”alisema.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Utawala, Kasper Mbuya, aliwapongeza wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wataalamu, kwa kazi nzuri ya kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Samia na kazi inayofuata ni uhakiki ili kupata takwimu halisi ya kilichotekelezwa.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa wakuu wa mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, alisema wakuu wa mikoa ndiyo timu ya ushindi katika shughuli zote za serikali zinazoelekezwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza, ilisema utekelezaji wa Anwani za Makazi ni mfumo wa msingi utakaowezesha uchumi wa kidijitali ulioanza kutekelezwa mwaka 2010.
NA MWANDISHI, DODOMA