WATU wawili mtu na mdogo wake wakazi wa Kitongoji cha Nyandege, Kijiji cha Kegonga, wilayani Tarime mkoani Mara, Menganyi (45) na Kerato Mwita (47), wamehukumiwa kwenda jela miaka mitatu na miezi sita kila mmoja, baada ya kukiri kupatikana na hatia ya kumuua Ryoba Masiaga bila kukusudia.
Ndugu hao walidaiwa kumchoma Masiaga na kitu chenye ncha kali kifuani ulipotokea ugomvi kati yao na marehemu wakati wakinywa pombe.
Wakisomewa hukumu hiyo juzi, katika kikao cha Mahakama Kuu Kanda ya Musoma katika Mahakama ya Wilaya Tarime na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Sedekia Kisanya, alidai tukio hilo lilitokea Novemba 28, 2020.
Mwanasheria wa Serikali, Mafuru Moses, alidai tukio la mauaji lilitokea Kitongoji cha Nyandege, Kijiji cha Kegonga wakati Menganyi na Kerato wakinywa pombe katika kilabu ya Ghati Ryoba ambapo ulitokea ugomvi baina yao na marehemu.
Moses alidai katika kuzuia ugomvi wahusika walitolewa nje ya kilabu na watuhumiwa walijaribu kuondoka, lakini ugomvi ulizuka upya kati yao na Masiaga na kusababisha kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani na ubavuni hatua ambayo ilisababisha kifo chake papo hapo, baada ya kutokwa damu nyingi.
Watuhumiwa walikiri makosa na kuomba kusamehewa kwa kujutia makosa yao waliyotenda huku wakidai mbali na kuzuiwa na kutolewa nje ya kilabu kuacha ugomvi, Masiaga aliwafuata na kuanzisha ugomvi upya hali aliyosababisha mauti kumkuta.
Pia walijitetea ambapo Menganyi alidai ana mke na watoto sita na Kerato akijitetea ana mke na watoto saba wakiwemo wanafunzi.
Mwanasheria wa Serikali Mafuru aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa kwa kitendo walichofanya cha mauaji ambapo familia ya marehemu imeathirika kumkosa ndugu yao.
Jaji Kisanya aliwahukumu watuhumiwa wote wawili kila mmoja kwenda jela miaka mitatu na miezi sita.
Katika kesi nyingine, Nyamhanga Getentani, mkazi wa Kijiji cha Koleri Mugumu Serengeti, alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu kwa kumjeruhi Juma Ntigira kwa kumkata na panga sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia ulemavu wa kudumu.
Na Samson Chacha, Tarime