RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inawapenda wafanyabiashara wadogo maarufu machinga na malengo yake inataka wawe wakubwa ili waweze kulipa kodi kwa serikali.
Pia, amesema serikali imetoa sh. bilioni 34 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa masoko mawili makubwa yatakayoweza kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 2300 katika soko kuu la biashara Kariakoo.
Rais Samia alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara ndogondogo waliopo katika ufukwe wa Coco mjini Dar es Salaam, ambapo alisema serikali inawapenda na kuwathamini.
Alisema serikali inapowapanga ni moja ya majukumu yao ya kuwathamini na wala haiwatengi kama watu wanavyovumisha kwa kuwa kinachofanyika sasa maeneo mbalimbali ya nchi kwa wafanyabiashara ni kuwapanga maeneo yenye staha.
‘’Nia yangu mie na serikali ni kuwaweka katika maeneo yenye staha ili mfanye biashara zenu na ninachokitaka katika serikali yangu mtoke katika umachinga muwe wafanyabiashara ili muweze kulipa na kodi’’alisema.
Alisema anafurahishwa na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwapanga wafanyabiashara mbalimbali katika eneo hilo, hivyo wataendelea kuwepo kwa ajili ya kufanya biashara zao.
‘’Endeleeni na mipango yenu ya kuwapanga maeneo mbalimbali, nimesikia mnataka kuwapeleka Jangwani, nendeni mkajenge soko kubwa ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao. Nawapongeza sana viongozi wa machinga kwa kutusikiliza’’ alisema.
Hivyo, alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuwapanga na kuwaweka katika mazingira mazuri na ndio maana ameamua kutoa kiasi cha sh. bilioni 34 kwa ajili ya ujenzi wa soko kubwa na kuliboresha lililopo la Kariakoo.
ZIARA DARAJA LA SELANDER
Katika ziara yake Daraja jipya la Selander, Rais Samia aliwapongeza wakandarasi wote wanaoujenga mradi huo kwa kusimamia kwa uweledi.
Rais Samia alihoji namna ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa km 1.03 litakavyohimili mabadiliko ya tabianchi na kupanda kwa kina cha bahari ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila alimweleza kuwa katika kingo za chini za daraja hilo wametumia kitambaa maalumu yenye uwezo wa kuzuia mmomonyokowaudongo hatua itakayoifanya daraja hilo kutopata changamoto yeyote ya mabadiliko ya kimazingira.

Akieleza juu ya mradi huo unaogharimu Tsh.bilioni 243, Mhandisi Mativila alisema hadi sasa daraja la Selander limekamilika kwa asilimia 98.44 na ujenzi wa Barabara unganishi imekamilika kwa asilimia 96.33 na mkandarasi tayari amekwisha lipwa sh.bilioni 201,459 sawa na asilimia 82.65.
Mhandisi Mativila alisema mhandishi mshauri wa mradi huo amelipwa sh.bilioni 4.9 sawa na asilimia 80 na fidia kwa mali na ardhi sh.bilioni 2.4.
Akizungumzia ushirikishwaji wa wazawa katika mradi wa Daraja la Selander, Mhandisi Mativila alisema ajira zilizopatikana kupitia mradi huo ni 960 ambapo kati ya hizo ajira 886 zilichukuliwa na wazawa sawa na asilimia 92 huku wataalamu kutoka nje wakipata ajira kwa asilimia nane pekee.
Akitoa mchanganuo wa ajira hizo ambazo zimewanufaisha wazawa, Mativila alisema wahandisi wa umeme, mitambo na mazingira pamoja na kada zingine walikuwa 110, wakadiriaji, wahasibu 13 na wapimaji sita, mafundi mchundo na wasaidizi wa kada mbalimbali walikuwa 830.

“Mradi umeendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa wataalamu wa kada tofauti ikiwemo wahandisi wazawa kutoka taasisi mbalimbali, kufikia sasa, walionufaika na mafunzo kupitia mradi huu ni wahandisi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wahandisi wahitimu 22 na wanafunzi wa vyuo 37, tunategemea mafunzo haya yatasaidia kujenga uwezo na ujuzi utakaolisaidia taifa letu baadae,”alisema.
HAMIS SHIMYE NA BARAKA LOSHILAA