DHAMIRA ya serikali kuhakikisha machinga wanavuka hatua ya kuwa walipakodi imeanza kuzaa matunda, baada ya uongozi wa kundi hilo kueleza mafanikio wanayopata, yakiwemo kuaminiwa na kukopesheka na taasisi za fedha.
Akizungumza na UHURU, Makamu Mwenyekiti wa Machinga Tanzania Bara, Steven Lusinde, amesema asilimia 75 hadi 85 ya machinga nchini wanakopesheka na taasisi za fedha, jambo ambalo linaashiria mafanikio katika ukuaji wao kiuchumi.
“Tunachoamini hata matajiri tunaowaona walifikia huko kwa kuwa wanakopa, kwa hiyo unapoona mtu anakopesheka maana yake anatoka katika ufukara wa kibiashara anakwenda kuwa mkubwa kibiashara,” alisema.
Amefafanua uwezo wa kukopesheka umetokana na mazingira bora yaliyowekwa na serikali kwa taasisi za fedha, hivyo kuwa na utaratibu wa kuwakopesha wafanyabiashara wadogo kwa riba nafuu.
Ameongeza kuwa, kupewa kipaumbele kwa kufanya shughuli zao katika maeneo maalumu kumewaongeza vipato na wengi wana dhamana ya kuweka ili wapate mikopo.
Amesema pamoja na hayo, kuna mbinu nyingine inayotarajiwa kuzinduliwa kwa ajili ya kuhakikisha kundi hilo la wafanyabiashara linakuza mitaji yao na kupanua wigo wa biashara, hatimaye kuwa walipakodi.
Lusinde amesema sehemu kubwa ya machinga wanajisajili kuwa na leseni za biashara, ambayo ni hatua moja mbele katika dhamira ya serikali ya kuwafanya wajasiriamali kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Kuhusu ziara ya Rais Samia Ulaya, Lusinde amebainisha, kujitokeza kwao kwa wingi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwa ajili ya kumpokea juzi, ni ishara ya shukurani kwake.
“Rais alipokuwa Ulaya alitutaja, hivyo tulikwenda kumpokea tukiamini ana zawadi yetu na baada ya mapokezi alisema ametoka huko lakini amekuja na zawadi yetu, tunaamini ana dhamira nzuri na njema na sisi, tumempokea kwa furaha na tupo pamoja naye,” alisema.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais Samia, kutoa matumaini kwa machinga kuhusu upatikanaji wa mikopo bila dhamana.
Katika mkutano wake na machinga jijini Dar es Salaami, alisema atazungumza na taasisi za fedha kuona uwezekano wa machinga kupata mikopo bila dhamana.
Pia, alieleza atakaa na kuangalia uwezekano wa fedha za Uviko-19, sh. bilioni tano kuwekezwa katika mfuko wa Machinga SACCOS.
Benki ya NMB imeingia makubaliano na Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) ili kuwapa mikopo, mafunzo na bima kwa ajili ya biashara zao.
Kwa mujibu wa NMB bima hiyo, itaanzia sh. 10,000 kwa mwaka na mnufaika atapata hadi sh. 500,000, huku bima ya sh. 60,000 atapata hadi sh. milioni 10 akipatwa na majanga yaliyoainishwa.
Na JUMA ISSIHAKA