WIZARA ya Kilimo imeweka mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima ndani na nje ya nchi kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kudumu kuhusu uhaba wa masoko kwa wakulima.
Katika kutimiza azma hiyo, wizara hiyo imefanikiwa kupata eneo la maonesho ya bidhaa za kilimo katika nchi mbalimbali zikiwemo Saudi Arabia na China kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inavyosisitiza umuhimu wa upatikanaji masoko kwa mazao ya wakulima ndani na nje ya nchi.
Aidha, imedhamiria kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa za masoko ya mazao ya kilimo, itatoa mafunzo kuhusu kilimo biashara na mifumo ya masoko kwa maofisa ugani 2,000 na wakulima 4,000 kutoka mikoa 26.
Akizungumza na UhuruOnline, Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, alisema juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda ambapo sasa wakulima wa zao ngano wameanza kupata uhakika wa masoko.
Alisema wizara hiyo imekutana na wanunuzi wa zao hilo na wamekubali kununua ngano yote inayozalishwa nchini, uamuzi ambao umechochea ongezeko la bei kwa wakulima kufikia sh. 800 kwa kilo.
“Tayari serikali imefanikiwa kupata soko la uhakika la ngano inayozalishwa nchini ambapo wanunuzi wa ngano wameridhia kabla ya kununua ngano nje ya nchi, watahakikisha wananunua kwanza ngano inayozalishwa nchini na ndio sababu wakulima wameanza kulima kwa wingi zao hilo,” alieleza.
ZAO LA SHAYIRI
Akizungumzia kuhusu soko la wakulima wa zao la shayiri, alisema wizara hiyo imeanza kuchukua jitihada za kuimarisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa wakulima wa shayiri nchini.
Alisema serikali ipo katika majadiliano na kampuni za bia ili kuwekeza katika kiwanda cha kimea chenye uwezo wa kusindika shayiri tani 35,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima.
Profesa Mkenda alieleza kuwa hatua hiyo itawezesha upatikanaji wa soko la uhakika wa zao la shayiri, hivyo kuongeza uzalishaji wa ndani.
ZAO LA ALIZETI
Alisema zao hilo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati ambayo yatasaidia kumaliza upungufu wa mafuta ya kula nchini na ndio sababu serikali imeanza mkakati wa wakulima kulima zao hilo kwa mkataba maalum na wenye viwanda.
“Katika kuimarisha kilimo cha mkataba cha zao la alizeti, wizara itaendelea kuwaunganisha wakulima na wasindikaji kisha kuandaa mazingira bora ya uwekezaji katika viwanda vya kusindika alizeti,”alieleza Mkenda.
NFRA NA CPB
Alisema katika mwaka huu wa fedha serikali imepanga kuimarisha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) kuwa na uwezo wa kununua zaidi mazao ya wakulima na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu wa fedha, NFRA inatarajiwa kununua tani 165,000 za nafaka ambazo zinajumuisha tani 150,000 za mahindi, tani 11,000 za mpunga na tani 4,000 za mtama kutoka kwa wakulima, vikundi vya wakulima na vyama vya ushirika.
Aidha, CPB inatarajiwa kununua tani 32,400 za mahindi, tani 21,600 za ngano, tani 7,200 za mbegu za alizeti, tani 4,608 za muhogo, tani 34,560 za mpunga na tani 1,440 za korosho kutoka kwa wakulima kwa ajili ya viwanda vyake vilivyopo katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Mwanza na Dares Saalaam.
Vilevile, CPB inatarajiwa kununua kwa wakulima mazao ghafi ya mahindi, alizeti, mpunga, maharage ya soya, ngano, korosho, maharage, mtama mweupe, ufuta na mbaazi.
Pia, wizara hiyo kupitia TANIPAC itajenga kituo mahiri cha mafunzo kwa wakulima na usimamizi wa mazao baada ya kuvuna kwa ajili ya kuwezesha masoko na kusambaza teknolojia za usimamizi na uchakataji wa mazao ya kilimo baada ya kuvuna.
“Tumesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo kwa wasafirishaji mazao ambapo wamekuwa wakikumbana na usumbufu wa magari kusimamishwa mara kwa mara,” alisema Profesa Mkenda.
Aliongeza kuwa: “Hali hii inasababisha mnunuzi kushindwa kupeleka magari kwenda kununua mazao ya wakulima kwa kuhofia usumbufu wa kusimamishwa mara kwamara.”
MITAJI
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa mitaji kwa wakulima, Profesa Mkenda alisema katika mwaka 2021/2022, wizara itafanya tathmini ya mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wawekezaji wengine katika sekta ya kilimo.
Alieleza kuwa hatua hiyo ina lengo la kuibua vizuizi na kuvitafutia majawabu kwa ajili ya kuimarisha ugharamiaji wa mazao katika mnyororo wa thamani.
Profesa Mkenda alieleza kuwa kazi hiyo itahusisha kuendelea kufanya uchambuzi wa mfumo wa kisera, kisheria na kikodi ili kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kujihusisha na shughuli za kilimo.
“Wizara imeunda kamati maalum inayohusisha viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Kilimo, taasisi za fedha, Mfuko wa PASS na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa ajili ya kupitia na kushauri namna bora ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya maendeleo ya kilimo,”alisisitiza Profesa Mkenda.
Na Bakari Mnkondo Na Mussa Yusuph