BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema halitasita kupendekeza kuchukuliwa hatua kwa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa na wa kamati za mazingira wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao katika kusimamia utunzaji wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji.
Pia, limesema litatumia nguvu ya kisheria katika kushirikiana na Wakuu wa Mikoa nchini ili kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kulinda na kutunza vyanzo vya maji.
Mkurugenzi wa NEMC, Samuel Gwamaka, amesema kamati za mazingira zilizoundwa hazifanyi kazi na kusababisha maeneo onevu ya vyanzo vya maji kuvamiwa na watu na kuanzisha makazi.
“NEMC hatutasita kupendekeza kwa mamlaka husika kuchukuliwa hatua kwa watu tutakaobaini hawatekelezi majukumu yao. Hizi kamati hazitekelezi majukumu yake ndiyo maana tumefika hapa tulipo,” alisema.
Gwamaka alisema baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa hawatekelezi sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na mipango miji kwa kuruhusu wananchi kujenga miji katika maeneo yanayoathiri vyanzo vya maji.
Alifafanua kuwa chemchem nyingi za maji zimetoweka baada ya kuvamiwa na shughuli za binadamu zikiwemo za kilimo na ukataji miti hovyo.
Alisema Baraza halitakaa kimya kuona kuna uharibifu wa ustawi wa mazingira na uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa nchi.
Gwamaka aliongeza kuwa makorongo yamejaa Dar es Salaam kutokana na kutozingatia ustawi wa mazingira kwa kundoa uoto ambao ulikuwa unatengeneza uhifadhi wa maji.
Alitoa wito kwa wananchi kutunza na kusimamia vyanzo vya maji ili kuepukana na changamoto ya ukosefu wa maji.
“Sehemu kubwa ya vyanzo vya maji ambavyo vimeharibiwa ni kutokana na wananchi kukosa elimu ya utunzaji sahihi na usimamizi wa mazingira.
Kuna watu wamekata miti hovyo. Watanzania hebu tujifunze kutunza mazingira, Rais hawezi kuzunguka kila sehemu kutuambia,” alisisitiza.
Na IRENE MWASOMOLA