KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP, kumetengeneza uimara na heshima kwa nchi na CCM ya sasa.
Mbali na vyama, pia amesema muungano wa Zanzibar na Tanzania Bara (Tanganyika) ni uamuzi wa kupongezwa uliofanywa na waasisi wa taifa ambao wanastahili kupongezwa na kuenziwa milele.
Shaka alieleza hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ofisi ya CCM, Wilaya ya Musoma Vijijini, mkoani Mara.
Alisema bila uamuzi huo wa kihistoria, maadui wa ndani na nje wangepata mwanya na wepesi wa kulivuruga taifa.
“Tunawapa heko waasisi wetu kwa uamuzi wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar baadae TANU na ASP kuungana mwaka 1977. Kwa kweli, lilikuwa pigo takatifu dhidi ya maadui wa kisiasa. Waasisi wetu kimsingi walitafakari kwa kina hadi kupitisha misimamo thabiti kwa maslahi ya taifa,” amesema.
Shaka amesema uamuzi wa kuunganisha vyama vya TANU na ASP, kumeiongezea CCM nguvu za kisiasa na kiuchumi, kuimarika utulivu wa ndani, kuongezeka mitaji, rasilimali watu na vyanzo vya mapato.
Amesema hatua ya kuunganisha vyama siyo tu ilikuwa ya kizalendo, bali pia ilifanikiwa kuzima ndoto batili za wasaka madaraka na kudhibitiwa kwa wanasiasa wakorofi ambao walishindwa kutekeleza mbinu chafu za uchochezi na usaliti.
Ameeleza kuwa, waasisi wa taifa walipima kwa ustadi wa kisiasa hatua iliyoifanya CCM ijikite na kushiriki moja kwa moja katika harakati za mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika na kufanikiwa kujiweka kando ya vita baridi ambayo iliigawa dunia Mashariki na Magharibi.
Kwa mujibu wa Shaka, kadri unaposoma vitabu vya historia na nakala za mapitio ya mapambano ya kisiasa, utayaona mataifa ya Afrika yalivyoendelea kusakamwa kwa mbinu chafu huku maadaui wa ndani wakitumiwa kuwa vibaraka ili kuvuruga ustawi wa amani na utulivu.
“Hatua ya kupiga marufuku mfumo wa vyama vingi kwa wakati ule kulizifunga njia za panya na milango ya vichochoroni. Sehemu kubwa ya mataifa ya Afrika baada ya kujitawala yalikubali chama kimoja yakihofia kuundiwa mizengwe na utapitapi wa kisiasa,” ameeleza.
FAIDA MIAKA 45 YA CCM
Amesema wakati CCM ikifikisha miaka 45 tangu kuzaliwa kwake, imefanikiwa kuwaunganisha wananchi, kusimamisha umoja na kuunda mtandao wa uendeshaji wa siasa zake kwa uwazi, uhakika na utendaji wa pamoja.
“Ni jambo la kujivunia kuwa na taasisi yenye mizizi mirefu ya kisiasa, kinachojiendesha kimfumo, kimaadili, kinidhamu na hata kutoa maamuzi mazito kwa mujibu wa katiba yake kanuni, miiko na taratibu zake,” amesema.
Shaka amesema wakati huu Tanzania ikiwa na vyama vingi vya siasa ni fahari kuwa na taasisi imara ya kisiasa (CCM), iliyoimarika, kuheshimika mbele ya uso wa dunia huku baadhi ya vyama vikishindwa kujiendesha kwa uwazi, vikikosa demokrasia ya ndani na viongozi wake wakifukuzana kibabe.
“CCM haimfukuzi kiongozi au mwanachama wake bila kumkusanyia ushahidi wa makosa yake kinyume yanayokiuka katiba, kanuni na taratibu. Pia iko tayari kuwapokea wanachama waliofukuzwa au wenyewe kujiondoa baada ya kukidhi matakwa yaliyowekwa kwa mujibu wa katiba ya CCM,” amesema.
CCM ilizaliwa Februari 5, mwaka 1977 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP, uamuzi huo ulitokana na vikao vya juu vya pande mbili hizo na kuazimia kuwa na Chama kimoja imara kitakachowaunganisha Watanzania na kuimarisha uchumi wa nchi.
Na MWANDISHI WETU, Musoma