Ni Historia nyingine muhimu iliyoandikwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada ya kukutana na wadau wake ambao ni Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kuwapa semina kuhusu mambo mbalimbali yanayofanywa na Mfuko katika kuijenga na kustawisha sekta ya hifadhi ya jamii nchini pamoja na kueleza dhamira yake ya kukuza maendeleo endelevu ya Taifa.
Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil mjini Zanzibar baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa jukwaa hilo uliokuwa na kauli mbiu isemayo “Uchumi wa Buluu na Mawasiliano ya Umma”.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema kupitia mkutano huo Mfuko ulitoa semina kuhusu majukumu ya msingi ya Mfuko ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta rasmi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Mshomba amesema Mfuko unaunga mkono jitihada mbalimbi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi makini wa Rais Dkt. Mwinyi hasa katika kutimiza dhana na muelekeo ya Serikali kupitia uchumi wa buluu.

Amesema Mfuko umedhamini mkutano huo kwa kutambua umuhimu wa jukwaa hilo hasa ukizingatia kuwa ulitumia mkutano huo kuwajengea uelewa wahariri hao wa vyombo mbalimbali vya habari kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa maisha ya sasa na baadaye.
Aidha, amesema Mfuko umevutiwa zaidi na ushirikiano mzuri uliopo na wadau wake wakiwemo wanahabari na kwamba ushirikiano huo utaendelea kuwa endelevu.
Akitoa mada kuhusu shughuli zinazofanywa na Mfuko, Meneja Usimamizi Mafao wa NSSF, James Oigo aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo dhana ya hifadhi ya jamii, majukumu, muundo panoja na NSSF.
Oigo pia aliwapitisha kwa kina wahariri hao kufahamu majukumu manne ya Mfuko na kueleza namna ambavyo Mfuko umezidi kusogeza huduma zake karibu na wanachama kupitia mifumo ya Tehama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alipongeza kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Mfuko hasa katika kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa Watanzania waliojiajiri kupitia sekta rasmi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine.
Alisema NSSF inafanyakazi kubwa na nzuri inayoonekana kwa kuunga mkono

juhudi mbalimbali za Serikali ikiwemo Serikali ya Zanzibar katika kutimiza dhana yake ya uchumi wa buluu.
Naye Mhariri wa habari mwandamizi ambaye pia ni mjumbe wa TEF, Bakari Kimwanga ameipongeza NSSF kwa kudhamini mkutano huo ambao umetoa fursa ya kuweza kufahamu mambo mbalimbali yakiwemo ya hifadhi ya jamii pamoja na sera ya Serikali ya Zanzibar ya uchumi wa buluu.

Awali, Mhariri mwanamizi, Jesse Kwayu aliwataka Watanzania hasa walioajiriwa katika sekta rasmi kuondoa fikra za kutaka kuchukua fedha zao mapema kwani wakifanya hivyo watapata tabu watakapofikia uzeeni.







