OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu umebaki kuwa sawa kama ilivyokuwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka 2020 kwa asilimia 4.0.
Hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na baadhi zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Oktoba mwaka huu zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba 2020.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma leo na Mkurugenzi wa sensa na takwimu za jamii, Luth Minja, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu fahirisi za bei za Taifa kwa mwezi Oktoba.
Amesema kutokana na mfumuko huo kuwa sawa inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu.
“Kwa mfano baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei mwezi Oktoba mwaka huu ikilinganishwa na mfumuko wa bei wa mwezi Oktoba 2020 ni pamoja na maharagwe kwa asilimia 5.5, dagaa kwa asilimia 3.9, maziwa ya ng’ombe kwa asilimia 5.1 na choroko kwa asilimia 2.3,”amesema.
Mkurugenzi huyo wa Takwimu za sensa ametaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwezi Oktoba mwaka huu zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba 2020 ni mavazi kwa asilimia 4.8, gesi ya kupikia kwa asilimia 2.8, mkaa kwa asilimia 3.9 na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7.
“Mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu umepungua kidogo hadi asilimia 3.9 kutoka asilimia 4.0 kwa mwaka ulioishia mwezi na mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba umebaki kuwa asilimia 4.1 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu,”amesema.
Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu Minja, amesema kwa upande wa Nchi ya Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu umepungua hadi asilimia 6.45 kutoka asilimia 6.91 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu .
“Kwa upande wa Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu umepungua pia hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu,”amefafanua Minja.
Na Happiness Mtweve,Dodoma